Na. Dennis Gondwe, DODOMA
DIWANI wa Kata ya Madukani, Prof. Davis Mwamfupe ametoa rai kwa kata yake kuwa mfano katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kusimamia nguzo nne zilizoasisiwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kauli hiyo aliitoa katika kikao baina ya viongozi waandamizi wa chama hicho iliwa ni maadhimisho ya miaka 46 ya kuzaliwa CCM kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kata ya Madukani jijini hapa.
Prof. Mwamfupe ambae pia ni Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma alisema “viongozi wa Kata ya Madukani hatuna budi kuzielewa na kuzizingatia nguzo nne zinazotumiwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika utekelezaji wa majukumu yetu ili kuyafikia mafanikio na kuwa na maendeleo endelevu. Rais amebainisha kuwa nguzo hizo zikitumiwa kwa usahihi zinaweza kutupa mafanikio ya kisiasa na kiuchumi. Nguzo hizo ni maridhiano, ustahimilivu, mageuzi na kuijenga upya Tanzania”.
Akifafanua nguzo ya maridhiano, alisema kuwa inawataka watanzania kuwa pamoja.
“Bila kujali tofauti zao za kisiasa, kuhakikisha utawala wa sheria, usawa na kutobaguliwa, fursa sawa kwa wananchi wote kujiendeleza kibinafsi, jamii na taifa kwa ujumla” alisema Prof. Mwamfupe.
Akiongelea imani ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alisema kuwa anaamini maridhiano hayawezi kupatikana mahali ambapo pana ubaguzi. “Maridhiano hayapo mahali ambapo kuna wanaokosa fursa na haki zao za kiuchumi na kiraia. Rais ana sisitiza kama taifa ni muhimu kuzitumia nguzo hizo nne katika kusukuma maendeleo” alisepa Prof. Mwamfupe.
Awali Afisa Mtendaji Kata ya Madukani, Neema Komba alisema kuwa kata yake inamitaa mitano ambayo ni Massi, Suluhu, Jamali, Kamili na Relini ambayo imeshiki katika kufanikisha maadhimisho ya miaka 46 ya kuzaliwa CCM.
Maadhimisho ya miaka 46 ya kuzaliwa kwa CCM katika Kata ya Madukani yalitanguliwa na tukio la kutembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kusalimia wagonjwa, kuwapa neno la faraja na kuwapatia zawadi mbalimbali.