**************************
Na Emmanuel J. Shilatu
Misingi mizuri iliyojengwa na waasisi wa Taifa la Tanzania Mwalimu Julius Nyerere (Tanganyika- Bara) na Abeid Amani Karume (Zanzibar – Visiwani) imesababisha Wananchi wa Tanzania kwa muda mrefu kuishi kwa amani na utulivu huku wakifanya mambo yao kwa uhuru bila ya kuingiliwa na mtu yeyote Yule.
Tofauti na mataifa mengine Watanzania wako huru zaidi kwenda kokote kule ndani ya nchi na hata kuishi au kufanya kazi ama biashara bila ya bughudha yoyote endapo taratibu na sheria zitazingatiwa vyema.
Hali hii ni tofauti na nchi nyingine zikiwemo za jirani kama vile Kenya, Kenya Rwanda, Burundi, Kongo na hata Uganda ambapo ukabila umetalaki kuanzia ngazi ya kijiji hadi Taifa lakini kwa Tanzania hakuna ubaguzi wa rangi,dini wala kabila.
Hiyo inatokana na uongozi imara, sera safi, upendo na kila aina ya ubora uliotukuka ndani yake kwa jamii ya kitanzania. Jambo linaloendelea kutia faraja ni kuwa tangu ianzishwe Chama Cha Mapinduzi (CCM) toka zao la TANU na ASP imeendelea kuwa ni chama kinachotawala na kuongoza nchi. Na siri yote ya mafanikio hayo ni kutokana na kuwa nguzo imara ambazo ni Wanachama, Ilani ya chama, na Viongozi wake.
Wanachama wake ambao ndio mtaji wa chama wapatao zaidi ya milioni 12 na mashabiki wapatao ama zaidi ya milioni 16. CCM ni chama kisichozingatia uwepo au hata harufu ya ubaguzi wa rangi, kabila au dini ya mtu.
Hatua hio imewafanya Watanzania wengi kuanzia vijana kwa wazee, wake kwa wanaume kujivunia kuwa wanachama makini wa chama chenye mtazamo chanya wa kuwavusha kwenye neema. Ili kuhakikisha CCM inapata makada wa aina tofauti bila ya kujali umri, jinsia ilianzisha jumuiya za wazazi, wanawake (UWT) na vijana (UVCCM) ambazo ni viungo muhimu vya chama katika kuwaweka watu wote pamoja na karibu na hivyo kuendelea kuwa chama cha kishujaa katika kuwakomboa watu wake.
Pia kuna suala zima la uwepo wa ilani ya uchaguzi ambayo ni mkataba baina ya chama na wananchi au viongozi na wananchi ambao ndio wapiga kura wenyewe kupitia ilani, CCM inatoa ahadi zake mbalimbali za kutekelezwa katika muda uliopangwa wa miaka mitano.
Ni wazi kwamba ahadi hizo zimekuwa zikitekelezwa kwa kiwango kikubwa na cha kuridhisha kiasi cha kufanya Watanzania waendelee kuwa na imani nayo kila uchaguzi unapowadia. Hii inajidhihirisha wazi katika chaguzi kuu mbalimbali zilizofanyika mara tatu 1995, 2000, 2005, 2010, 2015 na 2020 ambapo CCM iliibuka na ushindi wa kishindo.
Nguzo nyingine kuu ya CCM ni viongozi wake. Ndani ya CCM wenye dhamana ya chama ni wanachama wenyewe na wala si viongozi. Hali hii imesaidia kutokuwa na hata chembe au harufu ya umimi wa mtu kujiona kuwa ana haki miliki ndani ya chama au ni kiongozi wa maisha. Ikumbukwe kuwa CCM ina haki zote kwa kiongozi yeyote yule aliyetokana na CCM.
Hiyo ni ishara kwamba ni chama chenye misingi imara ya uongozi na ndio maana kumekuwa na mabadiliko ya mara kwa mara ya uongozi kwa kufuata misingi ya katiba ya chama. Kila baada ya mitano hufanyika uchaguzi wa viongozi wa mashina hadi Taifa na katika uchaguzi huo ndipo watu huingia na kutoka.
Aidha hali hii ni tofauti na vyama vingine nchini ambavyo walivyoviasisi ni viongozi wa kudumu hadi hii leo. Wanapoambiwa kuna uchaguzi baadhi ya viongozi hao kufanya mizengwe kwa wale wanaonyesha nia ya kuleta mabadiliko na hata kuwafukuza.
Kwa sasa CCM ipo chini ya Uenyekiti wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha CCM inaendelea kuongoza kupitia ridhaa ya Wananchi.
Ridhaa hii inatokana na CCM kuendelea kuwa na uongozi imara, sera safi, maendeleo bora na hivyo kuendelea kuwa tegemeo la kila Mtanzania anayependa haki na maendeleo pamoja na ustawi uliopo.
Nyakati zote CCM imeendelea kuwa mstari wa mbele kwenye mapambano dhidi ya maadui wakuu watatu ujinga, maradhi na umaskini hali iliyopelekea maendeleo makubwa chanya nchini.
Heri ya miaka 46 kuzaliwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).