Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo akizungumza na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Chakula Duniani (WFP) Bi. Sara Gordon – Gibson, mazungumzo ambayo yalijikita katika ushirikiano wa Serikali na shirika hilo katika masuala ya hifadhi ya mazingira, yaliyofanyika ofisini kwa Waziri, Mtumba Mtumba jijini Dodoma
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo akiwa katika picha ya pamoja na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Chakula Duniani (WFP) Bi. Sara Gordon – Gibson na wataalamu wa Idara ya Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais mara baada ya kumaliza mazungumzo mazungumzo ambayo yalijikita katika ushirikiano wa Serikali na shirika hilo katika masuala ya hifadhi ya mazingira, ofisini kwa Waziri, Mtumba jijini Dodoma
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo akiagana na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Chakula Duniani (WFP) Bi. Sara Gordon – Gibson mara baada ya kufanya mazungumzo, yaliyojikita katika ushirikiano wa Serikali na shirika hilo katika masuala ya hifadhi ya mazingira, yaliyofanyika ofisini kwa Waziri, Mtumba Mtumba jijini Dodoma Februari 03, 2023.
(PICHA NA OFISI YA MAKAMU WA RAIS)
………………………………………
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo Februari 03, 2023 amekutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Chakula Duniani (WFP) Bi. Sara Gordon – Gibson ofisini kwake Mtumba jijini Dodoma.
Katika Mazungumzo hayo, Dkt. Jafo amepongeza jitihada kubwa zinazofanywa na shirika hilo ya kusaidia mataifa yanayoendelea ikiwemo Tanzania ya kusaidia miradi ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Amesema dhamira ya WFP ya kusaidia katika upatikanaji na matumizi ya nishati mbadala itasaidia katika kupunguza na kuzuia kasi ya ukataji miti kwa ajili ya kutafuta kuni na mkaa.
Aidha, Waziri Jafo amemuelezea mwakalishi huyo namna Serikali inavyoshirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha kupanda miti na kuitunza ili kupambana na ukame ambao unaweza kusababisha wananchi kushindwa kulima na hivyo kukosa chakula.
Katika mazungumzo hayo pia viongozi hao wamejadiliana kuhusu namna gani shirika hilo linaweza kusaidia katika miradi ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Sisi kama Tanzania tunaendelea kushiriki katika mikutano ya COP (Mikutano na Mabadiliko ya Tabianchi) inayofanyika kila mwaka katika nchi tofautitofauti, hayo ndio matunda ya diplomasia ambayo Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameikuza,” amesema.
Kwa upande wake Bi. Sara amepongeza Serikali ya Tanzania kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais inayosukuma mbele ajenda ya utunzaji wa mazingira kwa shughuli mbalimbali ikiwemo zoezi la upandaji miti.
Amesema kwa kuwa chakula (mazao) na mazingira ni vitu vinavyoendana hivyo, wao kama WFP wako tayari kuona Tanzania inafaidika na mikakati ya shirika hilo ya kusaidia katika mapambano dhidi ya athari za madiliko ya tabianchi.
Pia Bi. Sara ameonesha dhamira ya kushirikiana na Tanzania katika kutafuta teknolojia bora ya kupikia ambayo ni rafiki kwa mazingira pamoja na kuunga mkono zoezi la upandaji wa miti katika maeneo mbalimbali. Kikao hicho kimehudhuriwa pia na wataalamu Idara Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais.