Wajumbe wa Kamati ya Kuishauri Serikali Ubora wa Nguzo za Umeme za Miti, wakipima kiwango cha unyevu kilichopo ndani ya nguzo za umeme za miti katika kiwanda cha Qwihaya kilichopo Kasulu, mkoani Kigoma ili kijiridhisha na ubora wa nguzo hizo wakati wa ziara yao iliyofanyika Februari 3, 2023 mkoani humo.
Katibu wa Kamati ya Kuishauri Serikali Ubora wa Nguzo za Umeme za Miti, mhandisi Edson Ngabo(aliyeinama) akiwaonyesha wajumbe wa kamati hiyo ukubwa na umri wa nguzo za umeme za miti katika Kiwanda cha Qwihaya, mkoani Kigoma ili kijiridhisha na ubora wa nguzo hizo wakati wa ziara yao iliyofanyika Februari 3, 2023.
Wajumbe wa Kamati ya Kuishauri Serikali Ubora wa Nguzo za Umeme za Miti, wakipata maelezo kutoka kwa mwendesha mitambo ya kukaushia nguzo za umeme za miti katika kiwanda cha Qwihaya,Kasulu mkoani Kigoma ili kijiridhisha na ubora wa nguzo hizo wakati wa ziara yao iliyofanyika Februari 3, 2023.
Sehemu ya kiwanda cha Nguzo za Umeme za Miti, katika kiwanda cha kilichopo mkoani mara, Wajumbe wa Kamati ya Kuishauri Serikali Ubora wa Nguzo za Umeme za Miti, walifanya ziara ya kukagua viwanda pamoja na nguzo zinazozalishwa kiwandani hapo
Wajumbe wa Kamati ya Kuishauri Serikali Ubora wa Nguzo za Umeme za Miti, wakikagua mazingira ya eneo la kiwanda cha nguzo na mbao cha Tarime mkoani Mara wakati wa ziara ya kukagua viwanda pamoja na nguzo zinazozalishwa kiwandani hapo Februari 2, 2023. Kutoka kushoto ni Thomas Mbaga Meneja Mdhibiti ubora wa nguzo Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Katibu wa Kamati ya Kuishauri Serikali Ubora wa Nguzo za Umeme za Miti, Mhandisi Edson Ngabo Wizara ya Nishati, na Negro Sanga Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa nguzo Tanzania,(kulia) na Mmiliki wa Kiwanda cha mbao Nguzo na Mbao cha Tarime, Peter Mwera wa pili kulia
Katibu wa Kamati ya Kuishauri Serikali Ubora wa Nguzo za Umeme za Miti, Mhandisi Edson Ngabo Wizara ya Nishati,(kulia) na Wajumbe wa Kamati ya Kuishauri Serikali Ubora wa Nguzo za Umeme za Miti, wakikagua nguzo za umeme za miti zilizorundwika pembeni ya barabara ili zitumike kusambaza umeme, wakati wa ziara ya kukagua viwanda vya nguzo pamoja na nguzo za umeme za miti, Februari 2 na 3, 2023 katika mikoa ya Kigoma na Mara.
…………………………………..
Na Zuena Msuya, Kigoma
Kamati ya kuishauri Serikali namna ya upatikanaji wa Nguzo bora za Umeme za Miti wamefanya ziara ya kukagua ubora wa nguzo zinazo tengenezwa na viwanda vya nguzo vilivyopo Mikoa ya Mara na Kigoma na kubaini mapungufu mbalimbali katika viwanda hivyo.
Kamati imewataka wamiliki wa Viwanda hivyo kuyafanyia kazi mapungufu yaliyobainika ili kupata bidhaa zilizo na viwango vyenye ubora unaotakiwa katika Soko la ndani na nje kwa ujumla.
Hayo yameelezwa na Katibu wa Kamati hiyo, Mhandisi Edson Ngabo, kutoka Wizara ya Nishati, kwa niaba ya Kamati hiyo.
Ziara hiyo ya Kamati imefanyika katika Kiwanda cha Mbao na Nguzo cha Tarime kilichopo katika Wilaya ya Tarime mkoani Mara na katika Kiwanda cha Nguzo cha Qwihaya kilichopo katika Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, Februari, 2 na 3, 2023.
Mhandisi Ngabo, amesema kuwa lengo la ziara hiyo ni kukagua na kuona changamoto zinazowakabili wenye viwanda ili Serikali iweze kuzifanyia kazi na kutoa ushauri kwa wamiliki wa viwanda hivyo namna bora ya kuboresha viwanda vyao ili vizalishe nguzo zenye viwango vya ubora unaotakiwa ili kukidhi soko la ndani na Nje.
Katika ziara hiyo kamati hiyo, imebaini kuwa katika kiwanda cha Qwihaya, baadhi ya vifaa vinavyotumika kupima ubora wa nguzo kiwandani havijahakikiwa na Shirika la Viwango nchini (TBS) kwa muda mrefu, hivyo kusababisha nguzo zinazopimwa na vifaa hivyo kuwa na ubora wenye mashaka.
Aidha kamati imebaini kuwa kiwanda hicho hakina vifaa vya kutosha vya kudhibiti ubora unaotakiwa.
Kufuatiwa hali hiyo, Kamati imemtaka mmiliki wa kiwanda hicho, kuhakikisha anaweka vifaa vinavyotakiwa na vilivyohakikiwa na TBS kwa mjibu wa taratibu zilizopo ili kuzalisha nguzo zenye ubora unaotakiwa, kabla ya hatua zaidi kuchukuliwa dhidi ya kiwanda hicho.
Mhandisi Ngabo, alieleza kuwa nguzo zinazozalishwa chini ya kiwango cha ubora unaotakiwa husababisha hasara kubwa kwa Serikali na kuleta usumbufu kwa wananchi katika kuwapatia huduma ya umeme wenye uhakika na unaotabirika kwa kuwa zinaharibika na kuoza ndani ya muda mfupi.
Baada ya Kamati kutembelea kiwanda cha Tarime ambacho bado hakijaanza uzalishaji kutokana na sababu mbalimbali, imemshauri mmiliki wa kiwanda hicho kutumia wataalamu wa ndani ili kuweza kukamilisha na kuboresha ujenzi wa kiwanda hicho.
Vile vile kamati imemshauri mmiliki wa kiwanda hicho, kuangalia uwezekano wa yeye kufanya biashara ya kuuza miti ya nguzo ambayo iko tayari shambani kwa viwanda vingine vinavyohitaji kwa kuwa ana mashamba makubwa na yenye miti mikubwa inayofaa kwa kutengeneza nguzo za miti za umeme.
Kamati imemhakikishia mmiliki wa kiwanda cha Tarime kuwa tatizo la umeme linalokikabili kiwanda hicho litakwisha tu endapo atawasilisha mahitaji halisi ya matumizi ya umeme unao hitajika katika kiwanda hicho.
“Tumefanya ziara ya kutembelea viwanda vya kuzalisha nguzo za miti za umeme, katika Mikoa ya Mara na Kigoma, tumebaidi mapungufu yaliyopo, tumewaelekeza wamiliki kurekebisha kasoro hizo ili waweze kuwa na viwanda bora vyenye kuzalisha nguzo zenye kiwango cha ubora unaotakiwa ili kukidhi soko na ndani na nje ya Tanzania,” alisema Mhandisi Ngabo.
Akizungumza na Kamati hiyo, mmiliki wa kiwanda cha Tarime ameiahidi Kamati hiyo kuwa atahakikisha ushauri huo anaufanyia kazi ili aweze kunufaika na mazao hayo ya miti.
Vilevile ameiomba Serikali kuwawezesha wawekezaji wa ndani ili waweze kuwa na viwanda vikubwa na kuzalisha nguzo bora kwa faida yao na Taifa kwa ujumla.
Aidha, kabla ya Kamati kuanza ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhandisi Innocent Luoga, aliwataka wajumbe wa Kamati hiyo kufanya kazi walizoagizwa na Serikali kwa weledi na kuzingatia miongozo waliyopewa kwani lengo ni kuhakikisha kuwa nguzo za umeme zinazotumika nchini zinakuwa na ubora unaotakiwa na ziweze pia kukidhi ubora unaohitajika katika soko la nje kutokana na uwepo wa nguzo nyingi zinazozalishwa nchini kutoshereza mahitaji ya ndani.
Miongoni mwa mambo aliyoyasisitiza Kamshna Luoga ni kuhakikisha kamati hiyo inakagua hatua kwa hatua mlolongo mzima wa uzalishaji wa nguzo kuanzia kwenye mashamba, viwanda, hadi katika matumizi.
Kamati hiyo inafanya ziara ya kukagua viwanda vya kuzalisha nguzo za umeme katika Mikoa ya Mara, Kigoma, Tanga na Dar es Salaam.
Kamati hiyo iliundwa Mwezi Aprili 2022, na Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba wakati alipofanya Mkutano na wadau wa kuzalisha Nguzo za miti za umeme katika Mikoa ya Iringa na Njombe.
Kamati hiyo inaundwa na Wajumbe 14 kutoka katika kila kundi la Wadau wa nguzo za miti za Umeme nchini, Wizara ya Nishati, Makatibu Tawala wa Njombe na Iringa, Wakala wa Nishati Vijijini( REA), Shirika la umeme Tanzania (TANESCO) na Shirika la Viwango nchini ( TBS) na wadau wa Mazao ya Miti.