Na Mwandishi wetu, Tabora
Mkuu wa Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora, Naitapwaki Tukai kwa mara ya kwanza tangu ateuliwe na Rais Samia Suluhu Hassan na kuapishwa na Mkuu wa Mkoa huo Balozi Dkt Batilda Salha Buriani, amezungumza na Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega na kujitambulisha kwao, kusalimiana na kutoa maagizo ya Serikali.
Halmashauri hiyo ina majimbo mawili ya Nzega Vijijini inayoongozwa na mbunge wake Dkt Hamis Kigangwalah na Bukene ya Suleiman Zed.
Amesema anamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa uteuzi huo na kuwaasa wampe ushirikiano ili kwa pamoja waweze kuwatumikia wana Nzega.
“Najua tutakutana katika Kata zenu ila nawaasa siwaagizi nachotaka ni kila mmoja acheze kwenye nafasi yake, Diwani asiingilie majukumu ya mtaalamu na wataalam washirikisheni madiwani kwani hao ndiyo walipmba kura kwa watu,” amesema DC Tukai.
Amesema jamii ya eneo hilo ihakikishe wanafunzi wote wanaopaswa kuanza shule na hawajaenda wanatakiwa waende shule na mwisho iwe baada ya wiki mbili.
“Waheshimiwa madiwani, suala la wanafunzi hasa wa kike kwenda shule litakuwa kipaumbele changu hivyo nitasimama kidete kwenye hilo,” amesema DC Tukai.
Amesema wananchi wanahitaji mazingira salama kwa ajili ya kutekeleza shughuli zao za kiuchumi hivyo matukio ya vitendo vya kihalifu, yanayotokana na Imani potofu yanapaswa kupigwa vita kwa kushirikiana na wananchi na vyombo vyote vya ulinzi na usalama na wadau katika wilaya,” amesema DC Tukai.
Amesema kwenye utunzaji wa mazingira na upandaji miti hivi sasa nchi inapita katika kipindi kigumu kutokana na mabadiliko ya tabia nchi unaosababishwa na uharibifu wa mazingira hasa ufyekaji miti, uharibifu wa vyanzo vya maji, uchafuzi wa mazingira na uchomaji moto.
Amesema vitendo hivyo vinaathiri sana mazingira na kusababisha ukosefu wa mvua, ukame na hivyo kupata mazao machache ya Kilimo.
Amesema amejipanga vyema kusimamia ukusanyaji wa mapato, kupitia Halmashauri zake mbili zlizopewa jukumu la kuwahudumia wananchi, zitimize lengo hilo, ni vyema halmashauri zisimamie makusanyo ya kodi na ushuru mbalimbali ili kuleta uwezo wa Halmashauri wa kutoa huduma.
“Hakikisheni mnatekeleza ilani ya uchaguzi wa CCM ya mwaka 2020 – 2025 waheshimiwa madiwani, Serikali iliyopo madarakani inatokana na CCM na ninyi mmetokana na chama hicho kasoro Diwani mmoja,” amesema DC Tukai.
Amewataja maafisa ugani wawatembelee wakulima kujua hali ya maendeleo ya mazao ya wakulima na kutoa ushauri; maafisa uwekezaji, biashara na viwanda, wahakikishe wanafanya kazi vizuri.
“Siri ya mafanikio ni ushirikiano, umoja na upendo, mimi nitawapenda sababu ni kiongozi wenu nanyi mnapaswa kunipenda na tufanye kazi kama timu,” amesema DC Tukai.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega Henerko Kanoga, amesema Nzega wanapenda umoja na mshikamano na watatekeleza maagizo yake.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega, Kiomoni Kibamba amesema wapo tayari kutekeleza maagizo, kuchukua ushauri na ushirikiano.
Diwani wa Kata ya Kasela, Regina Ndulu amemkaribisha Mkuu huyo wa Wilaya na kumuahidi kumpa ushirikiano wa kutosha.
Diwani wa Kata ya Mwantundu Paschal Rugonda amesema wanayo furaha kubwa kumpokea DC mpya aliyeteuliwa na Rais Samia.