Na Mwandishi wetu, Tabora
MKUU wa Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora, Naitapwaki Tukai amekabidhiwa ofisi na mtangulizi wake Kamishna msaidizi wa polisi (ACP) Advera Bulimba, hivyo kuanza rasmi majukumu yake mapya ya kuwatumikia watu wa Nzega.
DC Tukai amekabidhiwa rasmi ofisi hiyo February 3 na DC Bulimba ambaye amehamishiwa Wilaya ya Biharamulo Mkoani Kagera.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa ofisi yake amesema atahakikisha anaitunza Nzega kama alivyoikuta na ataendeleza pale alipoishia mtangulizi wake DC Bulimba.
“Kikubwa ni kushirikiana kwa pamoja ili kuhakikisha Nzega yetu yenye neema tele inazidi kupiga hatua na kusonga mbele kwenye suala la maendeleo, hodi Nzega,” amesema DC Tukai.
Amesema kila mtu aliyepo Nzega anampa Imani na kumpenda kwa asilimia 100 kwa kila mmoja atakayeonana ila zitapungua endapo yeyote atakayeshindwa kusimamia nafasi yake, hivyo washirikiane ila anapenda ukweli ulionyooka kuliko uongo.
“Lengo la Serikali inayoongozwa na CCM ni kuwatumikia wananchi hivyo tutimize wajibu wetu ipasavyo katika kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan ambaye namshukuru sana kwa kunipa hii heshima ya kuwaongoza wana Nzega,” amesema DC Tukai.
Awali, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Advera Bulimba ambaye amehamishiwa wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera amesema Nzega ina watu 592, 252.
Bulimba amesema wilaya ya Nzega ina majimbo matatu ya uchaguzi ya Nzega mjini ya mbunge Hussein Bashe ambaye ni Waziri wa Kilimo, Nzega vijijini ya Hamisi Kigangwalah na Bukene ya Suleiman Zed, Halmashauri mbili za Nzega mjini na Halmashauri ya Wilaya ya Nzega, Tarafa nne Kata 46, mitaa minne na vijiji 179.
“Katika uongozi wako tegemea kupewa ushirikiano wa kutosha na wana Nzega na pia kamati ya usalama itakusaidia mno kwani hao ndiyo wasaidizi wako wakubwa,” amesema DC Bulimba.
Hata hivyo, Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya hiyo (DAS) Evence Chambo amesema ofisi hiyo ina watumishi 18.