***********************
Na. WAF – Mbeya
Ilo kufanikisha Bima ya Afya kwa Wote, Upatikanaji wa dawa na vifaa tiba, Serikali kupitia Wizara ya Afya inaendelea kuwajengea uwezo watoa huduma za afya nchini kuweza kutoa huduma bora za afya kwa wananchi.
Hayo yamesema leo na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera wakati akifunga mafunzo ya Kuzuia na kudhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza kwa watoa huduma za Afya Jijini Mbeya.
Wakati akifunga mafunzo hayo Mhe. Homera amewasihi watoa huduma za Afya kuendelea kuwaelemisha wananchi ili wajiunge na Bima ya Afya itakapopitishwa na Bunge ili waweze kupata uhakika wa matibabu kabla ya kuugua.
Aidha, Mhe. Homera amesema Mafunzo haya yaliyofanyika sasa Jijini Mbeya ni awamu ya sita ambapo hadi kufikia leo hii jumla ya watoa huduma 460 kutoka katika vituo vya Afya 115 kutoka mikoa mitano ambayo ni Mbeya, Katavi, Iringa, Rukwa na Njombe.
“Ni matumaini yangu kuwa baada ya mafunzo haya, watoa huduma wetu mtaongeza ufanisi katika kutoa elimu kwa wananchi wanaokuja kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya ili wachukue tahadhari na kuepuka vichocheo hatarishi vya magonjwa yasiyoambukiza.” Amesema Mhe. Homera
“Natambua mafunzo haya ni muhimu sana katika utoaji wa huduma bora za magonjwa yasiyoambukiza kama vile magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, shinikizo la juu la damu, kisukari, saratani, sikoseli, afya ya akili na ajali.” Amesema
Mwisho, amewapongeza washiriki wote kwa kushiriki mafunzo hayo kikamilifu na kuweza kupata ubobezi katika kutoa elimu kwa jamii, kufanya utambuzi wa awali, uchunguzi na matibabu stahiki kulingana na ugonjwa husika.
Kwa upande wake Kaimu Meneja Mpango wa Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza – Wizara ya Afya Dkt. Asteria Mpoto amesema mikakati ya Serikali ni kuimarisha huduma za msingi kwa kuvijengea uwezo vituo vya Afya 600 nchini.
“Vituo hivi vya Afya 600 tunalenga Kuwapa mafunzo watoa huduma za Afya juu ya utoaji wa huduma za Kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza ambapo hadi kufikia 2023 watoa huduma 3000 tutakuwa tumewafikia.” Amesema Dkt. Mpoto
Mafunzo hayo yataendelea katika Mikoa iliyosalia ukiwemo Mkoa wa Ruvuma, Mtwara, Morogoro, Tanga, Manyara, Shinyanga na Tabora ambapo jumla ya watoa huduma 710 watafikiwa katika vituo 172 vya Mikoa hiyo.