Na Mwandishi wetu, Tabora
MKUU wa Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora, Naitapwaki Tukai amekula kiapo mbele ya Mkuu wa Mkoa huo Balozi Dkt Batilda Burian ili kuanza rasmi majukumu yake mapya ya kuwatumikia wananchii wa eneo hilo.
Mkuu huyo mpya wa Wilaya ya Nzega ambaye alikuwa mtumishi wa CCM makao makuu Dodoma aliteuliwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan January 25 kushika nafasi hiyo iliyokuwa inashikiliwa na Advera Bulimba ambaye amehamishiwa Wilaya ya Biharamuro Mkoani Kagera.
Akizungumza baada ya kuapishwa February 2 Nai amesema atahakikisha anashirikiana na wananchi wa Wilaya ya Nzega ili kufanikisha maendeleo.
“Kwa kushirikiana na wananchi pia tutahakikisha tunatekeleza maelekezo yaliyotolewa na Mhe Mkuu wa Mkoa kuhusu kukomeshwa kwa matukio ya vitendo vya ukatili,” amesema Nai.
Amesema atahakikisha pia wanasimamia utunzaji wa mazingira kwa kukomesha uharibifu wa mazingira unaofanywa na baadhi ya wananchi.
“Pamoja na kufanya ziara za kuwatembelea wananchi pia nitatenga muda wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi kwenye maeneo yao mbalimbali,” amesema Mkuu huyo wa Wilaya ya Nzega.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Balozi Dkt Batilda Burian amewaagiza wakuu wa Wilaya kushughulikia mauaji ya ushirikina na matukio ya ulipizaji kisasi kwenye maeneo yao ili wananchi wasiwe na hofu.
“Kumekuwa na baadhi ya matukio ya mauaji yanayotokana na sababu kadhaa zikiwemo ulipizaji kisasi, wivu wa kimapenzi, ujambazi na imani za ushirikina hivyo hakikisheni mnakomesha hayo,” amesema Balozi Dk Baruani.
Mkuu huyo wa Mkoa, pia amewaagiza wakuu hao wa Wilaya kushughulika na kukomesha uharibifu wa mazingira kwa kuhakikisha mazingira yanatunzwa ili kuwa na uhakika wa upatikanaji wa mvua na kutoharibu vyanzo vya maji.
Wilaya ya Nzega ina Halmashauri mbili za Mji wa Nzega na Halmashauri ya Wilaya ya Nzega.
Pia ina Wabunge wawili akiwemo Waziri wa Kilimo Hussein Bashe ambaye ni Mbunge wa Nzega Mjini na Dkt Hamis Kigangwalah Mbunge wa Nzega Vijijini.