WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Februari 2,2023 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kuhusu siku ya Kimataifa ya kupinga Ukeketaji dhidi ya Wanawake na Watoto wa kike Duniani.
Sehemu ya Waandishi wa habari na watumishi wa wizara hiyo wakimsikiliza Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima, wakati akitoa taarifa kuhusu siku ya Kimataifa ya kupinga Ukeketaji dhidi ya Wanawake na Watoto wa kike Duniani leo Februari 2,2023 jijini Dodoma
…………………………………
Na Alex Sonna-DODOMA
IMEELEZWA takwimu zinaonyesha kuwa ukeketaji nchini bado ni tatizo hali inayotokana na baadhi ya jamii zetu kuendelea kukumbatia mila na desturi zenye madhara na kuwadhalilisha watoto wa kike.
Hayo yamebainishwa leo Februari 2,2023 jijini Dodoma na Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Dkt Dorothy Gwajima, wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari hukusu siku ya Kimataifa ya kupinga Ukeketaji dhidi ya Wanawake na Watoto wa kike Duniani.
Waziri Gwajima amesema madhara hayo ni pamoja na kupoteza damu nyingi na kusababisha vifo, maambukizi ya VVU/UKIMWI na kusababisha matatizo wakati wa kujifungua.
Amesema Watoto wakati wa kukeketwa hushindwa kuhudhuria shule kwenye vipindi kwa muda mrefu na hivyo kuzorotesha maendeleo yao kielimu.
“Serikali kwa kushirikiana na Wadau inaendelea na jitihada za kukabiliana na vitendo vya ukeketaji kupitia mipango na mikakati iliyowekwa ikiwemo kutunga na kufanya marekebisho ya sheria na sera mbalimbali za nchi,” amesema Dkt Gwajima.
Amesema kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) ,inasisitiza usawa na heshima kwa binadamu wote,kutambua na kuthamini utu wa mtu pamoja na kuhakikisha haki mbele ya sheria.
Aidha amesema kuwa Maadhimisho hayo mwaka huu yatafanyika katika ngazi ya Mkoa kulingana na mazingira yao na kiwango cha hali ya ukeketeji katika mkoa husika ,hivyo Wakuu wa mikoa wana jukumu la kufanya maandalizi kuelekea siku hiyo.
“Natoa wito kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha maadhimisho haya yanafanyika ngazi zote kwa kuandaa Mdahalo wa Wadau wanaotekeleza shughuli za kutokomeza ukeketaji nchini pia kutoa elimu kwa jamii kuhusu madhara ya ukeketaji kwa njia ya mikutano ya hadhara, vikao na maandamano.”amesema
Amesema kuwa Kaulimbiu ya maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kupinga ukeketaji Duniani ni “Wanaume na Wavulana; Tushiriki Kupinga Mila na Desturi zenye Madhara ili kutokomeza Ukeketaji.
”Kauli mbiu hiyo inahimiza ushiriki wa wanaume na wavulana katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukeketaji ambayo ni kinyume cha Sheria na kinyume cha haki za binadamu.”ameeleza
Pia, amesema kuwa kaulimbiu inatambua umuhimu wa wanaume na wavulana katika kushawishi wanawake na watoto wa kike kutotamani kufanyiwa ukeketaji.
“Natoa wito kwa Wanaume na Wavulana kote nchini kubadili mitizamo na kuongeza jitihada katika mapambano ya kupinga ukeketaji dhidi ya Wanawake na watoto wa kike kwa kuwashawishi kutotamani kufanyiwa ukeketaji”amesema Gwajima
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Watoto Sehemu ya Familia Bi.Asha Shame amesema kuwa kwa sasa Tanzania ina asilimia 10 ya vitendo vya ukeketaji huku mikoa inayoongoza kwa vitendo hivyo ikiwa ni Manyara yenye asilimia 58,Dodoma ina asilimia 47,Arusha ina asilimia 41,Mara ina asilimia 32 na Singida ina asilimia 31.
Naye Mratibu wa Kutokomeza ukeketeaji Tanzania Bw.Denis Mose wakati akijibu swali kuhusu Mikoa inayoongoza kwa kuwa na wanaume wengi ambao hawajaingia tohara amesema kuwa baada ya kampeni iliyofanywa na Serikali kwa kushirikiana na mashiriki mbalimbali imesaidia mikoa ya Njombe,Iringa,Singida na Tabora Wanaume wengi kuingia katika vitendo hivyo vya tohara.
Februari 06, 2003 Baraza la Umoja wa Mataifa liliidhinisha kufanyika kwa Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukeketaji kwa Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa kwa lengo la kutokomeza vitendo vya ukeketaji kwa wanawake na watoto wa kike duniani Siku hii huadhimishwa kila mwaka tarehe 06 Februari.