Na John Walter-Manyara
Serikali imesema hadi kufika mwaka 2025 huduma ya maji safi na salama katika mkoa wa Manyara inatarajiwa kuwafikia wananchi kwa asilimia 85.
Hayo yamesema na mkuu wa mkoa wa Manyara Charles Makongoro Nyerere wakati akishuhudia utiaji saini wa mikataba ya miradi ya maji katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Manyara kati ya Wakala wa maji safi na usafi wa mazingira (RUWASA) na wazabuni waliopata tenda ya kutekeleza miradi hiyo ya maji uliofanyika katika ofisi za mkuu wa mkoa wa Manyara.
Makongoro amesema mpango wa kuhakikisha changamoto ya maji unatatuliwa Mkoa wa Manyara ni mpango wa serikali hadi kufikia mwaka 2025 hivyo amewaasa wazabuni pamoja na makampuni ya usambazaji waliosaini m ikataba ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maji mkoani manyara kufanya bidii ili ikamilike kwa wakati.
Aidha kutokana na changamoto ya ununuzi wa mabomba ya miradi ya mwaka 2022 Makongoro amesema zoezi hilo litafanywa na RUWASA na kazi ya wakandarasi itakuwa ni kutekeleza ujenzi wa miradi hiyo ili kuepusha usumbufu na changamoto zisizokuwa za lazima.
Miradi inayotarajiwa kutekelezwa na wakandarasi waliosaini mikataba ni miradi 28 ambapo miradi 7 ni mipya, miradi 8 ya kuongeza mitandao, visima 26 na usanifu wa miradi 53 kwa ujumla utekelezaji wa miradi hiyo utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 15 na milioni 406 ambazo tayari zimetolewa na serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania.
Kulingana na mikataba miradi hiyo inatarajiwa kukamilika mwezi desemba mwaka 2023 na itapunguza changamoto ya maji kutoka vijiji 91 hadi kufikia vijiji 51 na kukamilisha jumla idadi ya vijiji 40 vitakavyonufaika na miradi ya maji kwa mwaka huu ndani ya mkoa wa Manyara.
Baadhi ya vijiji hivyo ni Madunga, Utwari, Enoth, Lusinyai, Kiperesa, Esuguta, Aicho, Titiwi, Naberera, Losokonoi, Lobeno, Orkesmet, Luremo, Komolo, Olembere, Mogitu Gehandu..
Akizungumza kwenye hafla ya kusaini mikataba ya miradi hiyo, Meneja wa RUWASA mkoa wa Manyara Mhandisi Walter Kirita amesema kwa sasa wanahudumia asilimia 80 ya wakazi wa mkoa wa manyara hasa waliopo vijijini na huduma ya maji imefikia asilimia 64.3 sawa na ongezeko la asilimia 3.3 kutoka asilimia 61 mwezi juni mwaka 2022.
Akizungumzia Takwimu za utoaji wa huduma ya maji Mkoa wa Manyara, Kirita amesema wilaya ya Hanang ni asilimia 64, Babati asilimia 76, Kiteto asilimia 60.9, Mbulu asilimia 65.2 na Simanjiro ni asilimia 51.6.
Akizungumza kwa niaba ya wakuu wa wilaya, mkuu wa wilaya ya Babati Lazaro Twange amesema watasimamia miradi hiyo ikamilike kama ilivyopangwa na kumpongeza Raisi Samia kwa kuendelea kutekeleza miradi mbalimbali inayogusa wananchi wote kama miradi ya maji pia amewasisitiza viongozi wengine wote watoe ushirikiano kwa wakandarasi ili kuwasaidia panapotokea changamoto.
Nao wakandarasi na wazabuni wamesema wapo tayari kufanya kazi kwa bidii kama mikataba inavyoeleza kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati ili wananchi waweze kupata huduma ya maji safi na salama.