Tanzania inaendelea kushirikiana na nchi zinazounda Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA) kupitia utekelezaji Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA) na pia kupitia Utatu unaoundwa na nchi za COMESA, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk amesema hayo bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Momba, Mhe. Condester Michael Sichalwe aliyetaka kujua kwa nini Tanzania haioni haja ya kujiunga tena na COMESA.
Amesema Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi 19 zilizokuwa waanzilishi wa Jumuiya ya Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA) mwaka 1994. Hata hivyo, Tanzania ilijitoa katika COMESA mwaka 2000 kwa sababu ilikuwa ni mwanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambapo baadhi ya nchi za jumuiya hizo pia ni wanachama wa COMESA.
Ameongeza kusema Tanzania pia ilijitoa COMESA baada ya kujiridhisha kuwa nchi haitaathirika kiuchumi kwa kuwa bado ni mwanachama wa EAC na SADC na kwamba lengo ni kulipunguzia taifa gharama hasa michango ya uanachama kwenye Jumuiya hizo.
Pia amesema kitendo cha Bunge cha kuridhia kwa Mkataba wa kuanzisha Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA) hapo mwezi Septemba 2021, kunaifanya Tanzania kuendelea kushirikiana na nchi za COMESA.
“Ikumbukwe kuwa mwaka 2008 nchi za COMESA, EAC na SADC zilikubaliana kuanzisha Utatu na hivyo Tanzania inaendelea kushirikiana na COMESA kupitia Utatu huo wa COMESA–EAC-SADC,” alisema Mhe. Mbarouk.