NA STEPHANO MANGO, SONGEA
UMOJA wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Ruvuma wametakiwa wawe wapembuzi wa mada kwa umakini kabla hawajajenga hoja na kuzijibu hii italeta ukomavu mkubwa kwao katika kuelekea kipindi cha siasa za majukwaani
Wito huo umetolewa jana kwa nyakati tofauti na Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Ruvuma Kelvin Charles ambaye alikuwa Mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya miaka 46 ya kuzaliwa kwa Chama chama Mapinduzi wakati akitoa salamu za maadhimisho hayo yaliyofanyika wilayani Songea
Charles alisema kuwa maadhimisho ya mwaka huu yanapaswa vijana wakumbuke historia ya kuanzishwa kwa chama hicho na kuendelea kukifanya kibaki madarakani kwa kusaidia kero za wananchi zinatatuliwa huko kwenye mashina, kata na kwenye Wilaya ili wananchi waendelee kukiamini chama na kukibakiza madarakani
Alisema kuwa kila jambo ambalo unalifanya kijana linapaswa kuwa jema ili liweze kukuachia akiba ya kiuongozi huko mbele ya safari , kwasababu kesho njema ya kijana inatengenezwa leo kwa kila jambo ambalo unalifanya kwa maslahi ya Jumuiya, Chama na Taifa kiujumla
Akizungumza kwenye maadhimisho hayo Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana Wilaya ya Songea Mwalimu Joachim Komba alisema kuwa ili Jumuiya iweze kuendelea kutimiza wajibu wake kikamilifu inatakiwa tuungwe mkono na Chama ili tuweze kukilinda, kukisemea na kuhakikisha malengo yake ya kushinda na kuunda dola yanatimia
Komba alisema kuwa katika maadhimisho ya mwaka huu Jumuiya ya Vijana(UVCCM) inatakiwa ijitafakari sana kama malengo yake mahususi ya kikanuni na kikatiba kama yamefikiwa, hivyo sote kwa umoja wetu tujitathimini ili tuweze kusonga mbele zaidi
“Ikumbukwe vijana ndio injini ya chama hivyo, umoja wa vijana ukiwa imara ina maana na chama kinakuwa imara na kwamba umoja wa vijana ukiwaumedhoofika maana yake na chama kinadhoofika, hivyo tuna kazi kubwa sana ya kufanya ndani ya siasa za maridhiano kwa kuwashawishi vijana wengi kujiunga katika jumuiya na chama kwa ujumla wake “alisema Komba
Naye Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Songea Mjini Mwinyi Msolomi amewataka vijana hao kuwa huru kufanya shughuli za kisiasa kama maelekezo ya Chama, katiba na miongozo inavyotaka ili kuleta maendeleo kwa wananchi
Msolomi alisema kuwa vijana ndio tegemeo kubwa katika kufanikisha malengo ya chama hicho, hivyo wanapaswa kujiepusha sana na vitendo vya uvunjifu wa katiba na kanuni zake na kuacha tabia ya kuwa wapambe wa wagombea kabla na wakati wa uchaguzi
Kwa upande wake Katibu wa Jumuiya hiyo Wilaya ya Songea Mjini Witness Mwasanga alisema kuwa katika maadhimisho ya mwaka huu, UVCCM imefanya shughuli mbalimbali za kijamii na za kichama kwa lengo la kuhakikisha chama kinaendelea kuwa imara
“Tumepandisha bendera za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye mitaa mbalimbali , tumesajiri wanachama wapya, kushiriki ujenzi darasa shule ya msingi matarawe, ujenzi wa nyumba ya Mtumishi wa Uwt, pia tumepata darasa la Itikadi, siasa na uenezi kutoka kwa wakufunzi mbalimbali wa chama” alisema Mwasanga