Baadhi ya wanafunzi wa shule mpya ya Sekondari Majimaji kata ya Majimaji wilayani Tunduru wakiwa kwenye mapumziko.
Sehemu ya majengo katika shule mpya ya Sekondari Majimaji wilayani Tunduru kama yanavyoonekana.
Wanafunzi wa shule mpya ya Sekondari Majimaji wilayani Tunduru wakiwa Darasani,kwa mara ya kwanza kata ya majimaji imepata shule ya sekondari ambayo imesaidia kumaliza kero ya wanafunzi wanaotoka katika kata hiyo kutembea umbali mrefu hadi kata za jirani kufuata masomo.
Kaimu Afisa elimu sekondari wilaya ya Tunduru Stephen Makina, akizungumza na wanafunzi wa shule ya Sekobdari Majimaji alipokwenda kwa ajili ya kukagua mahudhurio ya wanafunzi waliochaguliwa kuanza masomo ya kidato cha kwanza katika shule hiyo.
Kaimu Afisa elimu sekondari wilaya ya Tunduru Stephen Makinajohn wa nne kushoto,akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya walimu wa shule mpya ya sekondari Majimaji na wajumbe wa kamati ya ujenzi wa shule hiyo.
………………………………………….
Na Muhidin Amri,
Tunduru
WANAFUNZI wanaomaliza elimu ya msingi katika kata ya Majimaji wilaya ya Tunduru na kuchaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari,wameondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kwenda kata ya Namiungo na Nakapanya kuendelea na masomo yao baada ya Serikali kujenga shule mpya ya Sekondari katika kata yao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo walisema,kabla ya serikali kujenga shule mpya wanafunzi wa kata ya Majimaji wanaochaguliwa kuendelea na kidato cha kwanza na kuendelea walilazimika kutembea umbali wa km 14 kwenda na kurudi shuleni umbali ambao ulikuwa changamoto kubwa na hivyo kusababisha kutofanya vizuri katika masomo yao na wengine kuacha shule.
Wameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuona umuhimu wa kujenga shule mpya ambao imewasaidia sana kupunguza kero ya kutembea na kutumia muda mwingi kwenda na kurudi shule.
George Expedito alisema, shule hiyo mpya itawawezesha kupata elimu yao karibu na makazi yao na kuhaidi kwamba watahakikisha wanatumia fursa kama waanzisilishi kufanya vizuri katika safari yao ya masomo yao.
Catherine Shaniel alisema,shule hiyo itawasaidia hasa wanafunzi wa kike kutimiza ndoto zao kwani wapo walioishia njiani na kuendelea na masomo kutokana na umbali wa kutoka nyumbani hadi shule.
Alisema,mara nyingi shule inapokuwa mbali wanaoathirika sana ni wanafunzi wa kike kwa kuwa wanakutana na vishawishi vingi barabara ikiwamo kupewa lifti na madereva wa magari na boda boda wanaotumia nafasi hiyo kuwalaghai na kufanya nao mapenzi na hatimaye kuacha shule kwa kupata mimba.
Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi wa shule hiyo Expedito Albano, ameipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kufanikisha kujenga shule hiyo ambayo itamaliza kero ya watoto wao kwenda kata za jirani kwa ajili ya kufuata masomo ya sekondari.
Alisema,mpango wa serikali ya kutoa elimu bure kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita na uboreshaji wa miundombinu ya shule ni fursa itakayowezesha watoto wengi waliopo kwenye kata hiyo kuendelea na elimu ya sekondari pindi wanapomaliza shule ya msingi.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa shule ya sekondari Majimaji Rashid Ching’anda,ameipongeza serikali ya awamu ya sita kutokana na uamuzi wake wa kujenga shule mpya ya Sekondari.
Alisema,kabla ya kujengwa kwa shule hiyo watoto wanaomaliza darasa la saba walikuwa na changamoto kubwa ya kwenda hadi shule ya sekondari Mtutura umbali wa km 7 na hivyo kusababisha baadhi yao kushindwa kuendelea na masomo kutokana na umbali uliokuwepo.
Alisema,kwa muhula wa masomo 2023 shule hiyo imepangiwa kupokea jumla ya wanafunzi 173 hadi sasa wanafunzi waliohudhuria kwa ajili ya kuanza masomo ya kidato cha kwanza ni 135 kati yao wavulana 78 na wasichana 57 huku wakitarajia kuwapokea wanafunzi waliobaki ndani ya wiki hii.
Alisema,wanafunzi waliopangiwa kusoma katika shule hiyo wanapokelewa kwa kadri wanavyokuja hata kama hawana mahitaji muhimu ikiwamo sare na vifaa vya madarasani kama agizo la serikali linavyotaka.
Hata hivyo ameiomba serikali kupitia Halmashauri ya wilaya Tunduru,wadau,jamii na wazazi kuunganisha nguvu zao ili kujenga nyumba za walimu na waweze kuishi karibu na sehemu yao ya kazi kwa sababu walimu wa shule hiyo wanaishi Tunduru mjini hivyo kuathiri sana utendaji wa kazi zao.