Na Shamimu Nyaki
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul Januari 25, 2023 Dodoma, amekutana na kufanya mazungumzo na Viongozi wa Shirikisho la Filamu nchini (TAFF) ambapo amewataka kuacha migogoro ambayo inapelekea kusimama kwa shughuli mbalimbali za Shirikisho hilo ikiwemo kufanyika kwa uchaguzi.
Mhe. Gekul amesema Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuboresha Sekta ya Sanaa ili wadau wake wanufaike na hivyo haipo tayari kuona malumbano yasiyokua na tija katika tasnia hiyo, akiwataka viongozi waliopewa dhamana katika Vyama na Mashirikisho ya Sanaa nchini kuheshimu Taratibu na miongozo iliyopo katika mashirikisho yao.
“Ukipewa dhamana ya kuongoza Taasisi au Chama chochote ujue umeaminiwa hivyo ni lazima ufuate Sheria, taratibu na Kanuni ambazo zinakuongoza katika kutekeleza majukumu yako bila kuonea wala kumuumiza mtu yoyote” amesisitiza Mhe.Gekul
Mhe. Gekul, ametumia kikao hicho kuiagiza Bodi ya Filamu, BASATA pamoja na Idara ya Maendeleo ya Sanaa kukaa na Viongozi wa Shirikisho hilo na Vyama vyake kwa lengo la kuzipitia na kuzifanyia marekebisho Katiba, Miongozo na Kanuni kwa ustawi wa Vyama na Shirikisho hilo mapema iwezekanavyo.