Picha mbalimbali za tukio la Mapokezi na mkutano wa Mjumbe wa Halmashauri Kuu CCM Taifa-Wazazi Hamoud Jumaa,katika mkutano na wanaCCM ofisi ya CCM wilaya na kikao cha Halmashauri Kuu CCM wilaya Kibaha Vijijini..
………………………….
Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
MJUMBE wa Halmashauri Kuu Chama Cha Mapinduzi Taifa (MNEC)-Wazazi ,Hamoud Jumaa amewaasa wanaCCM kujipanga kwenda majukwaani kusema makubwa yanayofanywa na Serikali ya awamu ya sita sanjali na utekelezaji wa ilani.
Ameeleza ,Rais Samia Suluhu Hassan ametoa fursa nzuri kuruhusu mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa ,hivyo ni wakati wa kutoka na kujibu hoja zinazoibuliwa dhidi ya Serikali.
Akizungumza na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM wilaya ya Kibaha Vijijini ,pamoja na baadhi ya viongozi na wanaCCM ,Kibaha Vijijini, Jumaa alieleza ,kusiwe na kigugumizi kukisema Chama ,wakati yapo yaliyotekelezwa na Rais dkt Samia na viongozi waliopita kwa miaka 46 ya CCM.
“Viongozi wenzangu, madiwani,wabunge na wanaCCM tutoke kusemea Chama na kupanda majukwaani kuitendea haki ilani ambayo utekelezaji wake unafanya vizuri”
Vilevile Jumaa alieleza ,miaka 46 ya Chama Cha Mapinduzi inatakiwa kubadilika ,na kufanya kazi na kuacha makundi ama kubezana wenyewe kwa wenyewe bila tija .
Aidha MNEC huyo alimpongeza Mwenyekiti wa CCM Taifa Dkt.Samia kwa kukisimamia Chama na kuendelea kuwa imara pamoja na kusimamia utekelezaji wa ilani kwa kufanya makubwa na kwa hakika anaitendea haki.
“Kwa miaka 46 wenyeviti wa Chama Taifa wamefanya sana ,Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere,Ally Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa,Jakaya Kikwete ,Dkt.John Magufuli na Tunashuhudia na kuona Dkt.Samia akitekeleza Yale yaliyoachwa na kuyaendeleza”
“Tushirikiane nae na kumuunga mkono kwa makubwa anayoyafanya katika sekta mbalimbali za afya,maji,elimu,viwanda na uwekezaji, miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo mradi mkubwa wa umeme Bwawa la Nyerere Rufiji, ujenzi wa madarasa na vituo vya afya “alifafanua Jumaa.
Pia amewaomba wanaCCM Kibaha Vijijini kushirikiana,kushikamana kwa umoja na kuacha kubezana ili kukijenga Chama na kujipanga katika chaguzi mbalimbali 2024 na uchaguzi mkuu 2025.
“Naombeni tuanze ukurasa mpya, tushirikiane,tuache siasa za kuombeana mabaya ,Tushawishiane katika chaguzi nani agombee ,nani anafaa na sio kubebana na kuwekeana visasi”alibainisha Jumaa.
Pamoja na hayo, aliwashukuru wanachama wote kwa kumwamini na kumchagua anachoahidi kufanya ziara mbalimbali, na kuonyesha ubora wake kwa kuwajibika kwa Watanzania na wanaCCM.
Nae Mwenyekiti wa CCM Kibaha Vijijini, Mkali Kanusu alieleza ,atatimiza majukumu yake na kusimamia utekelezaji wa ilani na miradi.
Awali Katibu wa CCM wilayani hapo, Safina Nchimbi alieleza, kama Chama walikuwa hajampokea rasmi MNEC ambae katokea katika wilaya hiyo ambapo wamempongeza kwa kuchaguliwa kwenye nafasi hiyo.
Safina alieleza, wanamshukuru kwa ahadi na Lengo lake la kujenga ofisi ya Chama na kusimamia ukarabati na ujenzi wa ofisi za kata kwani kwa kufanya hivyo ni kukiimarisha Chama .