Na Shamimu Nyaki – WUSM
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imeipongeza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kufanya mageuzi yenye tija katika wizara hiyo.
Pongezi hizo zimetolewa na Wajumbe wa Kamati hiyo wakati wakitoa maoni, ushauri na mapendekezo mbalimbali, baada ya kupokea Taarifa ya Utekelezaji wa Majukumu ya Wizara hiyo kwa kipindi cha Mwezi Julai hadi Desemba 2022, iliyowasiliswa na Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Pauline Gekul, Januari 24, 2023 Dodoma.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Stanslaus Nyongo amesema wizara hiyo imeendelea kufanya maboresho mbalimbali ambayo yanasaidia wadau wake kujiajiri, kupata kipato na zaidi kuchangamsha nchi kupitia sekta zake.
“Naipongeza sana wizara kama wajumbe walivyotangulia kusema, wizara hii sasa imepunguza maswali kutoka kwa wabunge, imekua wizara yenye tija kwa nchi, tunaona mafanikio katika sekta zake, michezo inafanya vizuri na inatangaza nchi, sanaa inazalisha matajiri wa umri mdogo na fursa nyingi zinaendelea kupatikana kupitia wizara hii” amesema Mhe. Nyongo.
Awali, Naibu Waziri Mhe.Gekul akiwasilisha taarifa hiyo ameeleza kuwa, katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2022, wizara imetekeleza mambo mengi ikiwemo kuratibu Siku ya Kiswahili Duniani, Mashindano ya Urembo na Utanashati kwa Viziwi, kuratibu ushiriki wa Timu za Taifa katika Mashindano mbalimbali ikiwemo Fainali za Kombe la Dunia za mpira wa Miguu Kwa Walemavu na Wanawake chini ya Miaka 17.
Mafanikio mengine aliyoyataja Naibu Waziri ni kutoa tuzo za filamu, kutoa tuzo za Uni Awards, kuratibu Mashindano ya Taifa Cup, na kushiriki tuzo za Black Entertainment Television ( BET) huko Los Angeles Marekani mwaka 2022.