Na Joseph Lyimo- Mirerani
MKURUGENZI wa kampuni ya Franone Mining & Gems Ltd, inayochimba madini ya Tanzanite eneo la Kitalu C, Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Onesmo Mbise, (maarufu kama Onee) ameitaka jamii isipotoshwe na maneno potofu kwani madini ya Tanzanite hayatoroshwi.
Mbise amezungumza hayo kwenye ziara ya Mkuu wa mkoa wa Manyara, Charles Makongoro Nyerere aliyetembelea machimbo ya madini ya kitalu C yanayochimbwa na watanzania wazawa.
Amesema watu wanaopotosha kuwa madini ya Tanzanite yanatoroshwa hawana nia njema na sekta hiyo kwani wanachonganisha wananchi na serikali kwa upotoshaji huo.
“Wanaosema madini ya Tanzanite yanatoroshwa, wanazusha kwani wachimbaji ni waaminifu na wanafuata maagizo yote kwa kupitisha kihalali kwenye lango la ukuta baada ya tathimini,” amesema Mbise.
Hata hivyo, amesema wanaishukuru serikali kwa kuiamini na kuwapa dhamana ya kuchimba madini hayo katika kitalu C na watachimba kwa uaminifu na kufuata sheria, kanuni na taratibu.
“Tunaishukuru serikali kwa kuiamini kampuni ya Franone ili ichimbe kitalu C ambapo inamilikiwa na watanzania watatu wazalendo, mimi, Vitus Ndakize na Matunda,” amesema Mbise.
Mkuu wa mkoa wa Manyara, Charles Makongoro Nyerere ameipongeza kampuni ya Franone kwa kushinda zabuni ya kuchimba kitalu C hivyo wanatarajia watafanikisha uchimbaji huo.
“Mmesema kampuni ya Franone ina wakurugenzi watatu wazalendo wa Tanzania tunatarajia mtaendesha shughuli zenu kwa uaminifu na kudhihirisha kuwa mnaweza,” amesema Makongoro.
Mwenyekiti wa CCM wa wilaya ya Simanjiro Kiria Laizer amesema wachimbaji wanamatarajio makubwa kwa kampuni hiyo ya wazalendo hivyo wahakikishe wanailinda imani hiyo.
“Mimi niliwahi kuwa ofisa rasilimali watu wa kampuni ya TanzaniteOne wakati wakichimba hapa kitalu C, hivyo hapa napaelewa mno nawatakia kila la heri,” amesema Kiria.
Mkurugenzi mwenza wa kampuni ya Franone, Vitus Ndakize amesema hivi sasa wanachimba mgodi mmoja kitalu C, pia wakifanya utafiti na lengo lao ni kuchimba migodi minne.
Ndakize amesema wakati wakiendelea na shughuli zao, wameandika mpango kazi wao kwa ajili ya kusaidia jamii inayowazunguka kupitia sekta watakayoafikiana.