Mkuu wa wilaya ya Tunduru Wakili Julius Mtatiro akizungumzia kuhusiana na mahudhurio ya wanafunzi waliochaguliwa kuanza elimu ya sekondari kwa mwaka wa masomo 2023.
……………………………….
Na Muhidin Amri,
Tunduru
SERIKALI Wilayani Tunduru,imetangaza msako mkali kwa wazazi na walezi wenye watoto ambao wamechaguliwa kuanza kidato cha kwanza kwa muhula wa masomo 2023 lakini hadi sasa bado hawajaripoti kwenye shule walizopangiwa.
Pia msako huo,utawahusu wazazi na watoto wenye umri na sifa ya kuanza elimu ya awali na msingi na waliokatisha masomo bila sababu za msingi na hivyo kusababisha kuongezeka kwa watoto wanaodhurura ovyo mitaani.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius,amesema hayo jana wakati akizungumza na Gazeti hili kuhusiana na hali ya mahudhurio kwa wanafunzi waliochaguliwa kuanza masomo ya kidato cha kwanza na elimu ya msingi mwaka 2023 katika shule mbalimbali wilayani humo.
“tutatumia week end hii(mwisho wa juma)kuwatafuta wazazi ambao bado hawajapeleka watoto wao shule ili watueleze kwanini watoto wao wako nyumbani,tutatumia sheria kuwafikisha mahakamani wazazi wasiopeleka watoto wao shule,hii nchi inaendeshwa kwa mujibu wa sheria,hivyo ni lazima tutumie sheria zilizopo”alisema Mtatiro.
Alisema wilaya ya Tunduru ni wilaya yenye mwamko mdogo wa elimu,hata hivyo kama viongozi waliopewa dhamana wataendelea kuhamasisha wazazi na jamii umuhimu wa kupeleka watoto shule ili kupata haki yao ya msingi.
Mtatiro ametoa wiki moja kwa wazazi na walezi kuhakikisha wanapeleka watoto shule na baada ya muda huo kupita serikali haitakuwa na huruma na mzazi au mlezi ambaye atabaki na mtoto wake nyumbani bila sababu za msingi na atafikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Aidha,amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na serikali yake ya awamu ya sita kwa kuipatia wilaya hiyo fedha za kutosha ambazo zimewezesha kujenga na kuboresha miundombinu ya elimu ambayo imesaidia sana wanafunzi kuwa na sehemu nzuri ya kujifunzia na walimu kufundishia.
Amewaagiza viongozi wa ngazi za vijiji,kata na Halmashauri kuwafuatilia watoto wote ambao hawajaanza kwenda shule na kuwataka wazazi kutoa ushirikiano kwa serikali iliyoonyesha dhamira ya dhati ya kuwajali wananchi kwa kujenga vyumba vingi vya madarasa.
Baadhi ya wakazi wa wilaya hiyo wamesema,kusua sua kupeleka watoto shule linatokana na hali ya kiuchumi kwani licha y serikali kuruhusu walimu kupokea wanafunzi bila ya kuwa na sale, ni vyema watoto kuwa na mahitaji yote muhimu.
Ali Sadala alisema, siyo kwamba wazazi hawapendi kupeleka watoto wao shule,isipokuwa changamoto za maisha zinachangia sana watoto kutokwenda shule kwa wakati.