Ofisa mipango wa halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Happiness Masatu akisoma rasimu ya mpango wa bajeti ya shiling bilioni 30 kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024 iliyopitishwa na Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya hiyo.
***************************
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, limepitisha rasimu ya mpango wa bajeti ya sh30 bilioni kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024.
Bajeti hiyo sh30 bilioni imeongezeka sh1.159 bilioni sawa na asilimia 4.1 ya bajeti ya mwaka 2022/2023 iliyokuwa sh28.8 bilioni.
Ofisa mipango wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Happiness Masatu amesoma rasimu ya bajeti hiyo mbele ya kikao cha baraza la madiwani lililofanyika mji mdogo wa Orkesumet makao makuu ya wilaya hiyo.
Masatu ametaja baadhi ya miradi ya wananchi itakayonufaika na bajeti hiyo ni kuwezesha sh99 milioni kwa vikundi vya vijana, wanawake na wenye ulemavu kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani.
Ametaja miradi mingine ni kujenga bweni shule ya msingi Saniniu Laizer kwa sh60 milioni, zahanati ya Olchoronyori sh10 milioni na sh6 milioni ya shule shikizi ya Songoyo – Loiborsoit.
Amesema sh4 milioni zitatumika kukamilisha vyoo shule ya sekondari Tanzanite, sh10 milioni za ukamilikaji wa nyumba shule ya msingi Naisinyai na sh10 za ukarabati wa madarasa shule ya msingi Songambele.
“Pia sh40 milioni za vitambaa vya mifugo kuzuia mbungo, sh10 milioni za choo sekondari ya Loiborsiret na ukamilikaji wa maabara ya shule ya sekondari Mirerani B.W. Mkapa kwa sh8.5 milioni,” amesema Masatu.
Amesema sh10 milioni zimetengwa kwa shule ya sekondari Eng’eno, sh10 milioni ukamilikaji wa nyumba ya walimu shule shikizi ya Irkinen Gunge na sh10 milioni sekondari Langai.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Baraka Kanunga amewasisitiza madiwani kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kuongeza tija kwenye miradi ya maendeleo.
Diwani wa Kata ya Orkesumet, Sendeu Laizer ameomba baraza hilo kubadili matumizi ya sh15 milioni ya ujenzi wa vyoo shule ya sekondari Simanjiro ili kujengea uzio wa shule hiyo.