Na Mwandishi wetu
MKUU wa Mkoa wa Manyara, Charles Makongoro Nyerere amempongeza Diwani wa Kata ya Mirerani Wilayani Simanjiro, Salome Nelson Mnyawi kwa kutoa fedha zake binafsi shilingi milioni 1 ya kutengeneza viti na meza za shule ya sekondari Tanzanite.
Makongoro ametoa pongezi hizo wakati alipofanya ziara ya kutembelea na
kukagua wanafunzi wapya wa kidato cha kwanza wa shule ya sekondari Tanzanite.
“Ninampongeza Diwani Salome kwa kutoa fedha zake mwenyewe shilingi
milioni 1 na kufanikisha ununuzi wa viti na meza hizo hivyo kuungana
na serikali kuboresha shule hiyo,” amesema RC Makongoro.
Hata hivyo amewataja wanafunzi wa kidato cha kwanza wa shule hiyo kuzingatia masomo kwa kusoma kwa bidii kwani wanasoma kwenye mazingira mazuri ya shule hiyo.
Diwani Salome amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha na kuwezesha ujenzi wa darasa jipya la shule ya sekondari Tanzanite.
“Pamoja na kumshukuru Rais Samia pia nampongeza Mkuu wa wilaya ya
Simanjiro Dkt Suleiman Serera kwa kufuatilia kwa ukaribu, ujenzi wa
darasa hili ambalo limekamilika,” amesema Salome.
Amesema ametoa fedha zake binafsi shilingi milioni 1 Ili kuwaunga mkono wananchi waliochangia kununua madawati mapya kwa ajili ya wanafunzi wapya wa kidato cha kwanza.
Mkuu wa shule ya sekondari Tanzanite, Jude Samwel Mziray amesema
darasa hilo limekamilika kwa gharama ya shilingi milioni 20 sambamba
na utengenezaji wa viti na meza 50.
“Viti na meza hizo zimetumia gharama ya shilingi milioni 3,750,000
ikiwa ni fedha za Diwani wa kata Salome Mnyawi na nguvu ya wananchi,”
amesema mwalimu Mziray.
Mwalimu Mziray amesema fedha hizo milioni 20 zimetumika kwenye msingi
na jamvi shilingi 6,436,000 ukuta shilingi 4,572,000 kupaua na kuezeka
shilingi 4,665,000 plasta na ripu shilingi 1,192,280 na umaliziaji
shilingi 3,134,720.
Amesema kuwepo na mradi huo wa chumba kimoja cha darasa umesaidia
kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani na wanamshukuru Rais Samia
kwa kuwaletea fedha hizo.
Ametaja changamoto walizokutana nazo ni ongezeko la gharama za vifaa
vya ujenzi kama kokoto, tofali, mchanga, na nondo na ngarama
kuongezeka kutokana na jiografia ya eneo la shule katika ujazaji wa
vifusi.
Amesema shule hiyo ina wanafunzi 618, wakiwemo wavulana 294 na wasichana 324 na endapo wanafunzi wote wakihudhuria shule hiyo itakuwa
na wanafunzi 1,107.