Jaji mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Songea Dkt Yose Mlyambina akiwaongoza watumishi na wadau wa Mahakama mkoani Ruvuma wakiwa kwenye maandamano kuashiria ufunguzi rasmi wa wiki ya sheria nchini ambayo kimkoa imefanyika katika viwanja vya soko kuu mjini Songea,nyuma ya Jaji Mlyambina ni Katibu Tawala wa mkoa Stephen Ndaki.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama kuu kanda ya Songea Dkt Yose Mlyambina akizungumza wakati wa maadhimisho ya wiki ya sheria nchini ambayo katika kanda ya Songea yanafanyika katika viwanja vya soko kuu mjini Songea
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanal Laban Thomas akizungumza wakati wa maadhimisho ya wiki ya sheria yanayoendelea katika viwanja vya soko kuu mjini Songea.
Mkazi wa Manispaa ya Songea ambaye hakufahamika jina lake mara moja,akisoma Ujumbe wa maadhimisho ya wiki ya sheria nchini ambayo katika mkoa wa Ruvuma yanafanyika kwenye viwanja vya soko kuu mjini Songea.
Baadhi ya wadau wa mahakama waliohudhuria uzinduziwa wiki ya sheria nchini ambayo katika mkoa wa Ruvuma inafanyika katika viwanja vya soko kuu mjini Songea.
******************************
Na Muhidin Amri, Songea
JAJI Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Songea Dkt Yose Mlyambina,amewataka mahakimu,majaji na wadau wengine wa sheria kutumia weledi katika kumaliza migogoro kwa njia ya usuluhishi badala ya kuwa sehemu ya kuongezeka migogoro na uhasama kwa jamii.
Jaji Mlyambina ametoa kauli hiyo leo,wakati akizungumza na watumishi na wadau wa Mahakama kwenye maadhimisho ya wiki ya sheria nchini ambayo katika kanda ya Songea yamefanyika katika viwanja vya soko kuu mjini Songea.
Amewaonya wadau hao,kuacha tabia ya kuwarubuni wananchi kukataa kumaliza migogoro kwa njia ya usuluhishi kwani kufanya hivyo ni kinyume na maadili ya kazi zao.
Jaji Mlyambina,amewaomba wananchi,kuhudhuria katika wiki ya sheria na kutembelea mabanda ya maonesho ili kupata elimu juu ya masuala ya sheria mbalimbali za nchi yao.
Aidha,ametoa wito kwa wananchi wa mkoa huo na maeneo ya jirani wenye malalamiko,maoni na mapendekezo ya uboreshaji wa huduma ya mahakama wafike kwenye maonesho ya wiki ya sheria ili kupata ufumbuzi na suluhisho la matatizo yao.
Ameeleza kuwa,wananchi watakaopata nafasi ya kutembelea mabanda ya mahakama watapata fursa ya kujifunza kwa kiasi gani mahakama ya Tanzania na wadau wengine ilivyojipanga kutoa haki kwa ufanisi na weledi mkubwa na kwa kiasi gani watapata haki zao.
Kwa mujibu wa Jaji Mlyambina, katika maadhimisho ya wiki ya sheria wananchi watapata elimu inayohusu msaada wa kisheria,ushughulikiwaji wa malalamiko mbalimbali na kupokea maoni na mapendekezo ya namna bora ya kuboresha shughuli za Mahakama na sekta nzima ya sheria,mifumo ya Tehama katika uendeshaji wa mashauri na maboresho ya sheria na kanuni.
Amewataka wadau wote wa mahakama kuhakikisha wanaongeza bidii katika kutatua migogoro na kumaliza mashauri yanayofikishwa mahakamani kwa njia ya usuluhishi badala ya njia ambazo hazimalizi badala yake zinaendeleza na kuongeza migogogoro katika jamii.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanal Laban Thomas amewataka wananchi wa mkoa wa Ruvuma, kujenga mazoea ya kutembelea maeneo yaliyoandaliwa kutoa elimu ya sheria ili wawe na uelewa mkubwa wanapotaka kufungua mashauri mahakamani.
Kanal Laban alisema, hatua hiyo siyo itawapa ufahamu mpana wa masuala ya sheria tu,bali itawasaidia kumaliza migogoro iliyopo kwenye jamii zao kwa njia ya usuluhisho badala ya kutumia nguvu na njia zinazokwenda kinyume na sheria za nchini.
“nawaomba sana wananchi wa mkoa wa Ruvuma,wawe na tabia ya kutembelea maeneo yaliyotengwa mahususi kwa ajili ya kutoa elimu ya sheria ili wapate uelewa mpana katika masuala ya sheria kwani itawasaidia kupata haki kwa wakati”alisema Kanal Laban.
Kanal Laban alisema,serikali imeshuhudia mabadiliko na maboresho mbalimbali yanayofanywa na mahakama hapa nchini ikiwamo usikiliza na utatuzi wa migogoro kwa wakati na kwa njia ya usuluhishi.
Mkuu wa mkoa, ameipongeza Mahakama kwa kufanya maonesho ya wiki ya sheria ambapo alisisitiza kuwa, maadhimisho hayo yataleta mabadiliko makubwa katika nchi yetu ikiwamo kumaliza migogoro ya ndoa,mirathi,madai na mengineyo kwa njia ya usuluhishi .