*******************
Na Mwamvua Mwinyi, Pwani January 22
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishna msaidizi Pius Lutumo , amefunga mafunzo ya utayari awamu ya tatu kwa askari wa mkoa na Wilaya huku akiwaasa kubadilika kwenye utendaji wa kazi zao kupitia mafunzo waliyopatiwa.
Mafunzo hayo yamefanyika kwenye viwanja vya mazoezi vilivyopo kwenye kambi ya Polisi Mkoa wa Pwani, Wilaya ya Kibaha, ambapo yamehudhuriwa na maofisa waandamizi wa ngazi ya Mkoa ,Wilaya pamoja na askari wa vyeo mbalimbali, askari 60 na walimu watano.
Msimamizi mkuu wa mafunzo hayo mrakibu wa Polisi ambaye ni mkuu wa kikosi cha Kutuliza Ghasia Mkoa wa Pwani ,Sija Kadogosa alieleza , kwa kipindi cha mwezi mmoja askari hao wameweza kujengewa uwezo katika Pivort drill, Tackticle Shooting, Stress Shooting, Vehicle Assolt & S.U.T, Weapon Training & Assemble kwa vitendo na matumizi sahihi ya silaha .
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani,Pius Lutumo aliwataka kutumia mafunzo hayo kama chachu ya mabadiliko ya utendaji ndani ya Mkoa kwa kwenda kuwatumikia wananchi na kuleta matokeo chanya.
Nae ofisa Mnadhimu Kamishna Msaidizi wa Polisi Mudhwari Msuya amewakunbusha askari waliomaliza mafunzo hayo umuhimu wa kufanya kazi kwa uweledi na hategemei kuona ofisi yake ikipokea malalamiko yatokanayo na huduma isiyoridhisha kutoka kwa jamii.
Aidha, askari Polisi Mkoa wa Pwani, wameweza kufanya usafi na kuchangia damu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi pamoja na kutoa vifaa vya usafi kwa wagonjwa waliolazwa katika wodi ya wazazi.
Miongoni mwa vitu vilivyotolewa ni sabuni, pampasi na vifaa vifaa vya kufanyia usafi (mafagio, sabuni za chooni na makwanja).
Akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Hospital ya Rufaa Tumbi, Dokta Feleciana Mmasi alimshukuru Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani na askari wote aliombatana nao katika Hospitali hiyo kwa kuona umuhimu wa kwenda kufanya usafi pamoja na kuchangia damu.