Serikali imeeleza kuwa, itaendelea kushirikiana na wadau wa Sekta ya Sanaa katika kuibua na kukuza vipaji vya Sanaa nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul katika hafla ya kumtambulisha Mwanamuziki Yammi ambaye ni Mpya na wa kwanza kwenye Lebo mpya ya Muziki iitwayo The African Princess inayoongozwa na Mwanamuziki Maarufu Bi. Faustina Mfinanga almaarufu Nandy, usiku wa Januari 19,2023 Dar es Salaam.
‘Sisi kama Wizara tunaahidi kushirikiana nanyi na ndio maana jioni ya leo tupo hapa, hivyo kwa wale ambao wana vipaji kama hiki cha Yammi msisite kutushirikisha kupitia vyombo vyetu mfano BASATA ili kila mwenye kipaji afike mbali” amesema Mhe. Gekul.
Mhe. Gekul ameeleza kuwa, Serikali inaendelea kuunga mkono jitihada za Wadau wa Sanaa nchini ambapo imefufua Mfuko wa Utamaduni na Sanaa ili kuwasaidia Wadau hao kuboresha kazi zao na kuwa za ushindani ndani na nje ya nchini.
Pamoja na mambo mengine Naibu Waziri huyo amempongeza Mwanamuziki Nandy kwa kuanzisha lebo ya Muziki na kuanza kusaidia Wanamuziki wengine, ambapo amemtaka kuendelea kusaidia Wanamuziki wengi hasa wa Kike.
Akizungumza katika hafla hiyo Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Dkt. Kedmon Mapana amemtaka Mwanamuziki Nandy kuongeza juhudi na ubunifu katika kazi yake ili aweze kuikuza lebo hiyo Kimataifa.
Aidha, amewataka Wanamuziki wengine kufuata Sheria katika kazi zao hususan kutambulika na Baraza la Sanaa la Taifa kwa kusajiliwa kama ambavyo amesajiliwa Nandy na Yammi.
Kwa upande wake Mwanamuziki Nandy ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kumuunga mkono katika hafla hiyo na ameahidi kuendelea kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha anapita njia sahihi katika Sanaa.
Vilevile ametumia fursa hiyo kuwaomba Wadau wa Sanaa nchini kumpokea na kuunga mkono kazi za Mwanamuziki Yamii, ambapo hadi sasa ameshatoa nyimbo tatu zikiwemo NAMCHUKIA, TUNAPENDEZANA, pamoja na HANIPENDI kupitia E P iitwayo THREE HEARTS.