Kaimu Jaji Mfawidhi wa mahakama kuu Kanda ya Tabora Dkt Mwajuma Kadilu akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Leo.
…………………………..
Na Lucas Raphael,Tabora
Mahakama kuu kanda ya Tabora imewaomba Wananchi kuhudhuria katika maadhimisho ya siku ya wiki ya kisheria ili kuweza kupata elimu kuhusu sheria na taratibu zinazotumika katika kuendesha mashauri.
Rai hiyo imetolewa na Kaimu Jaji Mfawidhi wa mahakama kuu Kanda ya Tabora Dkt Mwajuma Kadilu alipokuwa Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Januari 20, kwenye ukumbi wa Mahakama hiyo.
Alisema kwamba wananchi wanapaswa kupata elimu kuhusu sheria na taratibu zinazotumika katika kuendesha mashauri, ndoa na talaka, utekelezaji wa hukumu, Sheria za Watoto, taratibu za mashauri ya mirathi, msaada wa kisheria na ushughulikiaji wa malalamiko mbalimbali.
Jaji Dkt Kadilu alisema siku hii ya sheria nchini huadhimishwa kila mwaka kuashiria kuanza rasmi kwa shughuli za kimahakama kwa mwaka husika.
Alisema Siku hii itatanguliwa na Maadhimisho ya Wiki ya Sheria, yatakayoanza jumapili Januari 22 hadi tarehe 29 mwaka huu ambayo yatazinduliwa kwa Matembezi maalum yatakayoanzia viwanja vya mahakama kuu kuanzia saa moja na nusu kuelekea uwamja wa Chipukizi.
Dkt Jaji Kadilu aliongeza kuwa mgeni rasmi katika matembezi hayo, anatarajiwa kuwa mkuu wa Mkoa wa Tabora balozi Dokta Batilda Buriani.
Alibainisha kuwa kaulimbiu ya Wiki ya Sheria na Siku ya Sheria kwa mwaka huu ni UMUHIMU WA UTATUZI WA MIGOGORO KWA NJIA YA USULUHISHI KATIKA KUKUZA UCHUMI ENDELEVU ; WAJIBU WA MAHAKAMA NA WADAU
Kaimu Jaji Mfawidhi alisema elimu hiyo itatolewa na Mahakama na wadau wake mbalimbali wakiwemo ambao ni Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Chama cha Mawakili wa Kujitegemea, Tume ya Usuluhishi na uamzi, watoa huduma za msaada wa Kisheria, Takukuru, Polisi na Magereza.
Alisema kuwa Kilele cha siku ya Sheria Nchini itafanyika tarehe 01 Februari, 2023 katika viunga vya Mahakama ya mjini Tabora ambapo Jaji Mfawidhi wa Mahakama kuu kanda ya Tabora Amour Khamis anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.