Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza na Wadau walioshiriki uzinduzi wa Mradi wa USAID Kizazi hodari Jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mwanaidi Ali Khamis akitoa salaam kwa Wadau walioshiriki uzinduzi wa Mradi wa USAID Kizazi hodari Jijini Dodoma.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainab Chakula akitoa Salaam za Utangulizi muda mfupi kabla yakumkaribusha Mgeni Rasmi.
Kamishna wa Ustawi wa Jamii Dkt. Nandera Mhando akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mradi wa USAID Kizazi hodari Jijini Dodoma.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima akibonyeza kitufe kuashiria uzinduzi wa Mradi wa USAID Kizazi Hodari, wenye lengo la kuwasaidia vijana na watoto wanaoishi na VVU na katika mazingira hatarishi, hafla iliyofanyika Jijini Dodoma.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa Wizara za Kisekta wakati.wa uzinduzi mradi wa USAID Kizazi hodari, Jijini Dodoma
……………………
Na WMJJWM, Dodoma
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amezindua Mradi wa kuimarisha Afya, Ustawi na ulinzi kwa watoto na vijana wanaoishi katika mazingira hatarishi uitwao USAID Kizazi hodari katika hafla fupi iliyofanyika Jijini Dodoma Januari 17, 2023.
Akizungumza na washiriki wa hafla hiyo Waziri Dkt. Gwajima amewaelekeza Wadau wanaotekeleza Mradi huo ulioanza mwaka 2022, kutoa elimu sahihi ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto na kuendeleza programu za kuwaandaa wavulana kuwa wanaume bora wajao.
Ameelekeza pia kuendeleza utekelezaji wa shughuli za usimamizi wa mashauri ya watoto ili kutoa huduma kamilifu na endelevu na kuimarisha mifumo ya huduma za ulinzi na usalama wa Watoto katika jamii pamoja na kushirikiana na Mikoa na halmashauri kufanya ufuatiliaji wa huduma na kusimamia ubora wa takwimu vilevile.
“Mimi binafsi nitakuwa mstari wa mbele kwenda kwenye maeneo ya utekelezaji kuona maendeleo ya mradi huu. Aidha, katika kuboresha huduma za afya na ustawi wa jamii kwa watoto yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi pamoja na walezi wao, Wizara inaona vema afua hizo ziwekwe” amesema Dkt. Gwajima.
Ameongeza pia kwamba afua za mapambano ya ukatili wa kijinsia mashuleni ni muhimu sambamba na kufanya kazi kwa umoja wa dini mbalimbali (FCI) katika kukemea na kuibua matukio ya ukatili wa kijinsia.
Amesema afua nyingine ni kuboresha na kusambaza orodha ya watoa huduma za VVU/UKIMWI, ukatili dhidi ya watoto na ukatili wa kijinsia (Service Directory) pamoja n kuhuisha vikundi vya kiuchumi kwa ajili ya kuinua uchumi wa kaya miongoni mwa walezi na vijana balehe.
Akizungumza katika hafla hiyo, Askofu Mkuu wa kanisa la Kiinjili na Kiruteri Tanzania Dkt. Fredrick Shoo amesema huduma hizo za kusaidia Makundi ya Maalum ni za msingi zinazotambulisha kanisa.
“Taasisi za Dini zimeendelea kuwa Wadau wa huduma za kijamii hapa nchini. Kanisa la KKT limeendelea kutoa huduma hizi bila kujali Dini, kabila wala itikadi”.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mradi USAID Kizazi hodari Tanzania Dkt. Godson Maro amesema Mradi huo wa miaka mitano unalenga kuongeza utambuzi wa hali ya maambukizi ya VVU kwa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi, kuwaunganisha na huduma za Afya na uimarishaji wa huduma za usimamizi wa mashauri ya watoto.
Dkt. Maro ameongeza kuwa Mradi huo unaotekelezwa katika Mikoa 12 na Halmashauri 26 utaimarisha huduma za Kinga, tiba na matunzo kwa watoto walioathirika na VVU na ukatili wa kijinsia.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais TAMISEMI Bi. Amina Mfaki amesema uzinduzi wa Mradi huo ni ishara ya jitihada endelevu za kuboresha Afya na Ustawi wa watoto walioathirika na VVU na pia ni kielelezo Cha ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani.
“TAMISEMI inaendelea kutekeleza kupitia Mikoa na Serikali za Mitaa na huduma zinatolewa kwa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi, tukaendelee kusimamia kwa kushirikiana kwa maslahi ya Taifa letu”
Bi. Mfaki ameahidi kuwa maelekezo yote yaliyotolewa yatasimamiwa na kutekelezwa.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainab Chaula amesema uwepo wa Mradi huu utasaidia kuimarisha huduma kwa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi, ikiwa ni moja ya mipango na Sera zilizoandaliwa na Serikali.
Mradi huo unaolenga kunufaisha mikoa ya Kanda ya Kaskazini Mashariki na mikoa ya kusini, utagharimu Dola za Kimarekani takribani milioni 400.