Mgeni Rasmi katika Mafunzo ya Uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Wilaya Prof. Wakuru Magigi ambaye ni Mkurugenzi Mkuu Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi akifafanua jambo kwa wataalamu waliohudhuria mafunzo hayo tarehe 18/1/2023 Jijini Dodoma
Mratibu wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi Bw. Joseph Shewiyo akitoa ufafanuzi juu ya malengo ya mradi kwa wataalamu wa kada mbalimbali zinazohusiana na shughuli za uandaaji na upangaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi tarehe 18/1/2023 Jijini Dodoma
Mgeni Rasmi katika Mafunzo ya Uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Wilaya Prof. Wakuru Magigi ambaye ni Mkurugenzi Mkuu Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi akiwa kwenye picha ya pamoja na wataalamu wa kada mbalimbali zinazohusiana na shughuli za uandaaji na upangaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi tarehe 18/1/2023 Jijini Dodoma.
……………………………………..
Na Magreth Harrison na Halima Salum
Mkurugenzi Mkuu Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi Prof. Wakuru Magigi ametoa wito kwa wataalamu wa kada mbalimbali zinazohusiana na shughuli za uandaaji na upangaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi kuwa katika kutekeleza majukumu yao wazingatie sheria na taratibu za uandaaji wa Mipango ya matumizi ya ardhi katika ngazi ya Kitaifa na mipango ya matumizi ya ardhi ya Wilaya ili kuepuka migogoro ya ardhi.
Prof. Magigi alisema hayo wakati akifungua Mafunzo ya Uandaaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Wilaya yanayofanyika kuanzia tarehe 18 – 19 Januari 2023 katika Ukumbi wa ofisi za Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Jijini Dodoma.
‘‘Mipango ya matumizi ya ardhi Kitaifa pamoja na mipango ya matumizi ya ardhi katika ngazi ya Wilaya ni lazima yashabihane ili kuepuka migogoro ya matumizi ya ardhi baadae’’ alisema Prof. Magigi.
Prof. Magigi alifanua kuwa kuna sehemu zinajulikana ni mapito ya wanyama au ni misitu lakini inavamiwa na wananchi hivyo ni jukumu letu wataalam tusifanye makosa katika kuandaa matumizi ya ardhi ili kutunza rasilimali zetu tuongeze umakini katika upangaji kwa kulingana na matumizi ya maeneo husika.
Alieleza kuwa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi umeanza kuandaa muongozo wa matumizi ya ardhi ya Wilaya kwa kutoa mafunzo kwa wataalamu watakaohusika na uandaaji huo ili kila mshiriki awe na uelewa wa nini hasa anatakiwa kufanya katika utekelezaji wa Mradi huo mbao utapelekea kupatikana kwa hati milki za kimila 500,000 kutoka kwenye Halmashauri 7 za Wilaya ambazo ni Chamwino, Maswa, Songwe, Tanganyika, Longido, Mbinga na Mufindi.
Meneja Mradi katika maeneo ya Vijiji Bw. Joseph Hosena alisema kuwa kwa kupitia Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi mipango ya matumizi ya ardhi ya Wilaya 6 itaandaliwa, vijiji 250 vitapimwa mipaka yao, mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji 250 itaandaliwa pamoja na kuandaa mipango kina katika vitovu vya vijiji 250.
Bw. Joseph Shewio, Mratibu wa Mradi alisema kuwa wataalamu wawe na umakini pia katika kuangalia maeneo ambayo yananufaisha jamii kwa ujumla ili kuepuka migogoro katika jamii husika. Aliwaasa wataalamu kuwa wakiona vitu haviendi vizuri wapaze sauti kwenye vyama vyao vya kitaaluma ili kuepuka madhara ya baadae.
Mafunzo hayo kwa wataalam wa ardhi ni mojawapo ya hatua muhimu katika utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi ambao umelenga kuongeza na kuboresha usalama wa milki za ardhi nchini.