Na Dotto Mwaibale, Singida
MKUU wa Mkoa Singida. Peter Serukamba amewataka viongozi na watumishi wa Serikali Wilaya ya Iramba mkoani hapa kutekeleza wajibu wao kwa kufanya kazi ya kutoa huduma kwa wananchi kwa bidii na si vinginevyo.
Serukamba ameyasema hayo jana Januari 17, 2023 wakati akizungumza na wananchi wa wilaya ya Iramba ikiwa ni siku yake ya pili baada ya kuanzisha utaratibu wa kusikiliza kero zao ili kuzitafutia ufumbuzi kwa pamoja.
Alisema jambo kubwa aliloliona baada ya kusililiza kero hizo ni baadhi ya viongozi kushindwa kutekeleza wajibu wao ambapo aliwaomba watekeleze wajibu wao kwa kutoa huduma kwa wananchi ndio kazi yao.
“Kazi yetu ni kuwahudumia wananchi ukiwasikiliza mambo yote waliyoyasema hapa wala hayahitaji bajeti bali ni kusikilizwa na watu wanaojitoa kwa wenzao hivyo nakuomba mkurugenzi na wenzako haya yote tuliyo yabaini nendeni mkayafanyie kazi na jumanne mniletee mrejesho wa utekelezaji wake” alisema Serukamba.
Alisema hakuitisha kikao hicho kwa lengo la kusikiliza kero zao tu bali ni kuwasikiliza na kuzitatua kero hizo na kuwa zile ambazo hawatakuwa na uwezo nazo watazipeleka ngazi nyingine ya juu kwa ajili ya hatua nyingine na zile ambazo zipo ndani ya uwezo wao ni lazima wazitatue.
Serukamba alisema changamoto kubwa iliyojitokeza kutoka kwa wananchi hao ni ya migogoro ya arddhi ambapo alimuomba kamishna wa ardhi na timu yake kujipanga kwa ajili ya kutatua jambo hilo.
Alimwagiza kaimu mkurugenzi wa wilaya hiyo kusimamia haki ya wafanyakazi na alimuomba Afisa Utumishi kusimamia utekelezaji wa kazi kwa kufuata sheria na utaratibu uliowekwa wakati wa kutekeleza wajibu wao.
Alisema wananchi hao wanatarajia kusaidiwa changamoto walizo nazo ambazo sio kubwa lakini wao wamekuwa wakitumia muda mwingi kwenda kusimamia masuala ya kujenga barabara, madarasa lakini yale yanayowahusu watu hawashughuliki nayo.
“Mimi naamini watu hawa ambao changamoto zao hamzifanyii kazi ndio waliyoiweka Serikali iliyopo madarakani hivyo wangetamani kuona inatatua matatizo yao kupitia sisi tuliopewa dhamana ya kufanya hivyo baada ya kupekwa kufanya kazi ya kuwatumikia” alisema Serukamba.
Serukamba aliwaomba viongozi na watumishi wa wilaya hiyo kubadilisha mfumo wa kufanya kazi kwa mazoea badala yake uwe mfumo wa kutatua changamoto za wananchi ambapo alimtaka mkuu wa wilaya hiyo kwenda kwenye Tarafa, Kata na maeneo mengine kusikiliza changamoto za wananchi na kuwa ile tabia ya kufanya kazi bora iende wakati wake umepita.
Aliwatka wafanyakazi wa halmashauri hiyo kujiuliza wanapokwenda kazini kuanzia jumatatu hadi ijumaa kujiuliza wamefanya nini na wamewahudumia wakina nani na akaomba wawe na lugha nzuri kwa wanaowatumikia.
Aidha Serukamba aliagiza Halmashauri ya Wilaya ya Iramba kuhakikisha inaondoa takataka zote zilizopo kwenye maguba yaliyopo kwenye makazi ya watu na maeneo mengine ambapo alitoa ahadi ya kurudi kukagua maeneo hayo na wasije wakaelewana vibaya pindi atakapozikuta takataka hizo.
Baadhi ya kero zilizotolewa katika kikao hicho ni jinsi gani ya kulipwa fidia kwa mtu aliyeshambuliwa na tembo kero iliyotolewa na Hamphrey Philemon, Walimu wa Wilaya za Mkalama na Iramba ambao wana kidai chama cha akiba na mikopo cha Chamwai fedha zao waliochangia ili ziweze kuwasasidia baada ya kustaafu kero iliyowasilishwa na Mwalimu Zefania Makala, Uharibifu wa mazingira iliyotolewa na Janeth Mwendo, kutolipwa fidia kwa mmiliki wa eneo ilipojengwa Shule ya Sekondari ya New Kiomboi iliyotolewa na Stephano Juma.
Kero zingine ilikuwa ni malalamiko yaliyotolewa na Paul Alphonce aliyedai kulipia kupata huduma ya maji akiwa na wenzake ambao walitoa Sh.150,000 kila mmoja lakini hadi leo hii bado hawajafkishiwa huduma hiyo, kero nyingine ilitolewa na Mjasiriamali Anna Kizinga ambaye aliomba kupunguzwa kwa ushuru katika minada kutokana na biashara zao kuto nunuliwa, kero nyingine ilikuwa ni kukithiri kwa uchafu katika baadhi ya maguba yaliyopo mjini Kiomboi iliyotolewa na Zabron Malecela, kero ya kupelekewa mbolea ya ruzuku ambayo wakulima hawajaizoea iliyotolewa na Elia Zefania.
Kero nyingine iliyotolewa ni iliyowahusu watu wenye ulemavu wilayani humo ambao wanaidai halmashauri ya wilaya hiyo fedha za kujikimu walipokwenda kwenye maadhimishoya siku ya watu wenye ulemavu.
Kero nyingine iliyotolewa ilitolewa na Frank Nkundi ambaye anadai fidia ya kupata ajali akiwa kazini na Michael Juma ambaye anaidai halmashauri hiyo Sh, Milioni 1.3 kama kiinua mgongo baada ya kustaafu.
Kikao hicho kilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Taasisi za Serikali mkoani hapa, pamoja na wakuu wa idara ili kuzisikiliza na kuzitafutia ufumbuzi ambapo kikao kama hicho kitafanyika katika wilaya zote ambapo leo Januari 18, 2023 kitafanyika Wilaya ya Mkalama.