NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Chuo kishiriki cha elimu Dar es salaam DUCE kimewasilisha matokeo ya mradi wa Utafiti ujulikanao kama GATE ambao umeripotiwa kuwa utawajengea uwezo wanataaluma katika utafiti wa masuala ya jinsia ambao umefadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Ireland kwa miaka minne .
Akizunguzumza wakati wa uwasilishaji wa matokeo ya utafiti huo leo Jumatano Januari 18, 2023 Rasi wa Chuo Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE), Prof.Stephen Maluka amesema kuwa utafiti huo umekua na tija haswa katika kuwajengea uwezo wanataaluma kufanya tafiti zinazohusiana na masuala ya kijinsia ambazo zitaleta mchango mkubwa kwa Taifa.
Amesema kuwa utafiti huu utasaidia sana kwenye masuala ya kijinsia kwasababu umetoa mafunzo kwa wanafunzi kuhusiana na uwajibikaji na kuyaelewa masuala ya kijinsia na kubainisha kwamba umetoa mafunzo kwa wafanyakazi kutoka sehemu mbalimbali.
Kwa upande wake Dkt.Pepetua Urio ambaye ni kiongozi wa mradi huo amesema lengo la mradi huo ni kuhakikisha wanataaluma wanafanya tafiti zinazohusiana na masuala ya kijinsia zitakazoenda kusaidia jamii katika mambo mbalimbali.
Naye Dkt. Ikupa Moses Mkuu wa kitengo cha masuala Mtambuka Chuo cha DUCE na mtafiti mkuu katika mradi wa GATE ametoa wito kwa madawati ya kijinsia kutokata tamaa juu ya masuala ya kijinsia na kuendelea kutoa elimu kwa jamii.