***********
Na Mwamvua Mwinyi,Mafia January 17
UJENZI wa kipande cha barabara ya ‘Kichangachui – Hatchery’ kinachojengwa kwa kiwango cha lami Mjini Mafia ambao ulikuwa umekwama kwa takriban mwaka mmoja, upo mbioni kukamilika.
Ujenzi huo ulikwama kwa kipindi kuanzia Januari mwaka 2021 na unatarajiwa kukamilika wakati wowote kuanzia Sasa.
Taarifa iliyotolewa na Meneja wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) wilayani Mafia Mhandisi Francis Mugisha ,alieleza Mkandarasi G6 hatimaye amekamilisha uwekaji lami katika kipande hicho chenye urefu wa kilometa 0.9 ambacho ujenzi wake umegharimu kiasi cha sh.milioni 904,989,500.
Alieleza , Kazi zilizobaki kwa sasa ni ujenzi wa mifereji ya maji pembeni mwa barabara, kazi ambazo tayari Mkandarasi imeanza taratibu za utekelezaji.
Mkuu wa Wilaya ya Mafia Mhandisi Martin Ntemo , akikagua maendeleo ya mradi huo alielezea kuridhishwa na viwango vya ujenzi na kuitaka TARURA kuhakikisha suala la mifereji linakamilika kabla ya mvua za masika kuanza mwezi Aprili mwaka huu.
“Tunatambua changamoto zinazomkabili mkandarasi wanaotekeleza miradi hapa kisiwani Mafia hasa kwa upande wa usafirishaji wa vifaa kutokana na kibuko cha MV Kilindoni kuwa katika matengenezo kwa takriban mwezi mmoja hadi sasa” alieleza Ntemo.
Maelezo ya Picha Na.0141
Mkuu wa Wilaya ya Mafia Mhandisi Martin Ntemo(mwenye suti katikati)akikagua ujenzi wa barabara ya Kichangachui – Hatchery ambayo inajengwa kwa kiwango cha lami.
Maelezo ya Picha Na.0140,0139
Meneja wa TARURA wilayani Mafia Mhandisi Francis Mugisha (Kushoto) akimpatia maelezo Mkuu wa Wilaya ya Mafia Mhandisi Martin Ntemo, (mwenye suti )kuhusu utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya Kichangachui – Hatchery ambayo inajengwa kwa kiwango cha lami