Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET), Dk. Ellen Otaru akifafanua jambo wakati wa mafunzo .Dk. Elikana Kalumanga, Meneja Ushirikishwaji wa Sekta Binafsi wa Mradi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) wa Tuhifadhi Maliasili akiwasilisha mada ya uhifadhi wa bioanuai.
Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) akiongea na waandishi wa habari wakati akifungua ramsi mafunzo ya siku mbili kwa waandishi wa habari 25 Bagamoyo, mkoani Pwani.
********************
Na Sidi Mgumia, Bagamoyo
Ushirikishwaji wa viongozi katika ngazi zote unatajwa kuwa ni moja ya masuala muhimu katika kusaidia juhudi za uhifadhi wa shoroba na mazingira kwa ujumla.
Ushirikishwaji huo unapaswa kuwagusa wadau wote wa mazingira ili kuleta maendeleo endelevu ya malaisili zilizopo.
Hayo yamesemwa na Meneja Ushirikishwaji wa Sekta Binafsi wa Mradi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) wa Tuhifadhi Maliasili Dk. Elikana Kalumanga alipokuwa akizungumza wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini yaliyofanyika mjini Bagamoyo mkaoni Pwani.
Dk. Kalumanga amesisitiza kuwa ikiwa wadau muhimu kama vile Wizara ya Maliasili na Utalii, watunga sera, waandishi wa habari na wengineo wakishirikiana kwa pamoja katika maandalizi ya sera, mipango na michakato ya usimamizi wa mazingira itasaidia kulinda, kuhifadhi, kutunza na kusimamia mazingira kwa ajili ya kizazi cha sasa na cha baadaye.
“Pamoja na ushikishwaji wa viongozi na wadau wengine wa mazingira, bado elimu zaidi inahitajika kuwajuza wananchi juu ya masuala ya umuhimu wa maeneo yanayounganisha hifadhi mbalimbali nchini (shoroba), na hii ni haswa kwa wale wanaoishi kando ya hizo shoroba.
Hata hivyo kupitia mafunzo hayo yaliyoratibiwa na Chama cha Waandishi wa Habari wa Mazingira Tanzania (JET) chini ya ufadhili wa USAID, Mwenyekiti wa JET, Dk. Ellen Otaru amewataka waandishi wa habari kuwa mstari wa mbele kuibua na kuelimisha jamii juu ya athari zitokanazo na shughuli za kibinadamu kama kilimo na nyinginezo ndani ya shoroba pamoja na faida za kiuchumi zinazopatikana.
Akizungumzia juu ya mafunzo yanatolewa kwa waandishi wa habari za mazingira, Mkurugenzi wa JET, John Chikomo alisema ongezeko la watalii wanaoingia nchini ni mafanikio yanayotokana na elimu ya uhifadhi wa mazingira na wanyamapori inayotolewa mara kwa mara kwa waandishi wa habari hapa nchini.
“Ni vyema kwa waandishi kuelewa kwa undani mausala ya shoroba ili kuandika habari kwa kina na iwe rahisi kufikisha ujumbe kwa ufasaha kwa jamii, hivyo kupitia semina hii waandishi watafahamu faida zinazotokana na uhifadhi na utunzaji wa hizo shoroba,”alisema Chikomo.