***********
Na E. Kayombo WAF – Dar Es Salaam
Serikali itaendelea kutoa kipaumbele kwenye afya ya Mama na Mtoto kwa kuboresha ubora wa Huduma za Afya ya Mama na Mtoto na kuzisogeza karibu zaidi kwa wananchi.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu leo alipokuwa akifungua Mkutano wa Afya ya Mwanamke Barani Afrika unaofanyika hapa nchini katika Jiji la Dar Es Salaam.
“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kutoa kipaumbele na kutenga rasilimali fedha kwa ajili ya kuboresha huduma bora za jamii ikiwemo Huduma za Afya ya Mama na Mtoto ili kuifanya jamii iwe na maisha bora na hususani kuwaondolea usumbufu wanawake katika kupata huduma hizo” Amesema Waziri Ummy.
Waziri Ummy amesema kuwa Serikali imeimarisha miundombinu ya utoaji wa huduma za afya ya msingi pamoja na kuongeza idadi ya vituo vya afya ambapo huduma za afya zinapatikana karibu zaidi na wananchi.
“Hadi kufikia Januari 2023 jumla ya vituo vya afya 685 vimekarabatiwa au kujengwa ambapo vituo 421 ambavyo ni sawa na asilimia 61.4 vimeanza kutoa huduma ya upasuaji wa kumtoa mtoto tumboni” amefafanua Waziri Ummy Mwalimu.
Amesema katika kuimarisha huduma hizo za msingi Hospitali za Wilaya 102 zimejengwa na kukarabatiwa ili kuimarisha mifumo ya Rufaa za matibabu pamoja na kusogeza karibu na wananchi huduma za kibingwa.
“Katika kuondoa unyanyasaji wa mtoto wa kike, mwaka 2021 Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Tanzania aliruhusu watoto wa kike walioacha masomo kutokana na changamoto mbalimbali ikiwamo ujauzito kuendelea na masomo baada ya kujifungua” amesema Waziri Ummy Mwalimu na kuongezea kuwa viashiria vikubwa vya afya ya Mama na Mtoto vinahusiana kwa ukaribu na kiwango cha elimu.
Waziri Ummy amesema kuwa Suala la mimba za utoto bado ni changamoto kubwa hapa nchini hivyo kuwakata Wazazi, Walezi na Jamii kwa ujumla kutilia mkazo suala la elimu ya afya ya uzazi ili waweze kujitambua na kujikinga dhidi ya mimba za utotoni na magonjwa ya zinaa.
Aidha Waziri Ummy amesema kuwa Seta ya Afya inakabiliwa na uhaba wa asilimia 50 ya watumishi wa kada za afya hivyo kuwaomba wadau wa maendeleo ya Sekta ya Afya kushirikiana na Serikali katika kuziba pengo la watumishii wanaohitajika ili kuweza kulinda afya ya mama na mtoto.
“Tunawaomba sana wadau humu ndani mnapoandaa maandiko yenu kwenda kwa wafadhili muweke na kipengele cha kusaidia watumishi kada za afya wakiwemo watumishi wa afya ngazi ya jamii wote wana mchango mkubwa katika kuhakikisha wanalinda afya ya mama na mtoto” amefafanua Waziri Ummy.
“Tunaamini kabisa tukimwekea mwanamke mazingira rafiki zaidi kwa ajili ya afya yake ataweza kushiriki katika uzalishaji mali, malezi na matunzo ya watoto lakini pia ataweza kushiriki katika kuimarisha afya yake” amesema Waziri Ummy Mwalimu.