Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Viongozi wa Serikali wa Mkoa wa Ruvuma, kwenye Ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Januari 08, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
********************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wakuu wa wilaya na waganga wakuu wa mikoa yote nchini wasimamie maadili kwa watumishi wa sekta ya afya ili fedha zinazotolewa kwenye sekta hiyo ziendane na ubora wa huduma zinazotolewa kwa watanzania.
Amesema kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuhakikisha anatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya afya, ununuzi wa dawa na vifaa tiba, hivyo dhamira yake hiyo ni lazima iendane na ubora wa huduma zinazotolewa wa watumishi katika sekta ya afya.
Ameyasema hayo leo Jumapili (Januari 8, 2023) wakati akizungumza na viongozi wa Serikali wa mkoa wa Ruvuma, kwenye ukumbi wa Mikutano wa Manispaa ya Songea.
Pia, amewaagiza wakuu wa wilaya wasimamie upatikanaji wa dawa kutoka Bohari Kuu ya Dawa (MSD) na Busket Fund kwani Mheshimiwa Rais Dkt. Samia anatoa fedha za ununuzi wa dawa “Hatutaki kusikia malalamiko, Serikali kila mwezi inaleta fedha za ununuzi wa dawa, wakuu wa wilaya simamieni hili.”
Katika Hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka Wakuu wa wilaya kwa kushirikiana na Wakurugenzi na Maafisa Elimu wasimamie dhamira ya Mheshimiwa Rais. Dkt. Samia ya kutoa elimu bila malipo kaunzia darasa la awali hadi kidato cha sita kwa kutembelea katika shule na kukagua fomu za kujiunga na shule na kujiridhisha hakuna michango ya hovyo.
Aidha, ameagiza kuwepo na usimamizi wa shughuli za ustawi wa jamii ikiwemo masuala ya kiuchumi na kwa wafanyabiashara wadogo, wakati na wa kubwa. “Ni lazima tusimamie mwenendo wa uchumi kwenye jamii zetu, shughuli ambazo zinawaingizia kipato wananchi lazima tuzisimamie na kuziimarisha, lazima tufanye tathimini kama tunafanya vizuri au la, na lazima tujikite kwenye maeneo yote ikiwemo vijijini.”
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amesema viongozi katika halmashauri zote nchini ni lazima waweke utaratibu na tujikita katika kuondoa kero za wananchi pamoja na kuwa na dhana ya ushirikishwaji kwa kuwaeleza kila kinachofanyika Serikalini kwa kutumia vyombo vya habari na kufanya mikutano. “Lazima tufahamu kero zao na kusimamia kuzitatua.”
Akizungumza kuhusu makusanyo kwenye Halmashauri nchini Waziri Mkuu ameagiza kufanyike utambuzi wa vyanzo vyote vya mapato na kiasi cha fedha kinachoingiza na kuwataka wenyeviti wa halmashairi zote nchini na Mameya kuliwekea nguvu eneo la makusanyo.
Pia ameelekeza kuwa fedha zote zinazokusanywa katika vyanzo vyote ni lazima zipelekwe benki kabla ya kuingizwa kwenye matumizi. “Ni muhimu pia kukagua matumizi ya vyombo vyetu ya ukusanyaji wa mapato, fanyeni tathmini za mara kwa mara ya mwenendo wa makusanyo.”
Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Festo Dugange amesema kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia analeta fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa huduma za jamii na miradi ya maendeleo katika halmshauri hivyo viongozi katika maeneo hayo wanapaswa kusimamia fedha hizo. “Tunapaswa kusimamia na ni wajibu wetu kufanya hivyo ili tulete matunda yaliyokusudiwa na dhamira ya Rais kwa Watanzania iweze kufikiwa”