Mratibu wa Miradi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Trees for the Future Tanzania Mkoa wa Singida Ibrahim Mghama, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Upandaji miti ili kulinda vyanzo vya maji na uhifadhi wa mazingira mkoani hapa ulioongozwa na Mkuu wa Mkoa, Peter Serukamba uliofanyika jana katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida Ilongero.
Na Dotto Mwaibale, Singida
SHIRIKA lisilo la Kiserikali la Trees for the Future Tanzania
linalojishughulisha na kilimo mseto, kilimo endelevu kwa wakulima wenye kipato
cha chini vijiji ili kutokomeza njaa, Umaskini na Ukataji wa miti lenye makao
yake makuu mkoani Singida limetoa miche 3,000 kwa ajili ya kampeni ya kupanda miti ili kulinda vyanzo vya maji na kutunza mazingira iliyozinduliwa jana na Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi
wa kampeni hiyo iliyofanyika makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya
Singida Ilongero Mratibu wa Miradi wa shirika hilo Ibrahim Hassan Mghama alisema
miche hiyo ikiwemo ile wanayoigawa kwa wakulima imetolewa na shirika hilo kwa
kushirikiana na wadau wao Taasisi za
kiraia za Adese na Waendelee zote za Singida.
Mghama alisema tangu shirika hilo lianze kufanya kazi mkoani hapa mwaka
2016 limeshiriki katika matukio kadhaa likiwemo la upandaji wa miti Msitu wa
Mughola mwaka jana huku mwaka 2019 lilifanikiwa kupanda miti 2.5 milioni,
mwaka 2020 miti milioni 3.2.
” Tangu shirika hili lianze kufanya kazi limepanda miti zaidi ya 8 milioni
ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa Bustani Msitu ndani ya Mkoa wa Singida,”
alisema Mghama.
Alisema katika miti hiyo iliyopandwa ipo miti ya matunda, mbao, uzio, miti
ya kurutubisha ardhi na malisho kwa ajili ya mifugo.
Mghama alisema mwaka huu wamejipanga
kupanda miti milioni 3 na kuwa mpaka sasa wana miche takribani Milioni mbili na
laki tisa iliyopo kwenye vitalu 211 na kuwa lengo lao ni kupunguza umaskini wa
kipato kwa kufanya shughuli endelevu za upandaji wa miti ili kukomesha njaa,
umaskini wa kipato na kuboresha afya za wanajamii na uhifadhi wa mazingira.
Alisema kati ya miche hiyo 570 itapandwa kando ya barabara ya Singida
kwenda Mwanza, mingine itapandwa maeneo ya Karakana na kwenye chanzo cha maji
cha Mwankoko jumla ikiwa ni 1500.
Mghama alitumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi kuitunza miti hiyo inayopandwa
kwenye maeneo yao na kuacha tabia ya kuacha mifugo kwenda kuiharibu..
Kwa upande wake Msimamizi Msaidizi wa Miradi wa Shirika hilo, Nurudin
Kambulage alisema mkakati wa shirika hilo kwa mwaka huu ni kupanda miche mingi
zaidi ambapo kwa wadau wao wana zaidi ya miche milioni moja hivyo wakulima watapata ya kutosha na kuweza
kuhifadhi mazingira na ardhi katika mashamba yao.Msimamizi wa Miradi Msaidizi wa shirika hilo Mkoa wa
Singida, Nurudin Kambulage akizungumza kwenye uzinduzi huo.
mkoani Singida na wadau wao kutoka mashirika ya Adese na Waendelee wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kushiriki zoezi la upandaji miche ya miti.