Mwenyekiti wa Soko la Kiloleli Kalala Magafu akizungumzia namna ambavyo baadhi ya Wafanyabiashara wameacha vibanda vyao na kwenda kufanya biashara kwenye maeneo yasiyo rasmi
Baadhi ya Wafanyabiashara katika soko la Kiloleli wakiendelea na shughuli zao za kujipatia kipato.
**********************
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Wafanyabiashara ndogondogo halmaarufu kama machinga wanaofanyia shughuli zao katika soko la Kiloleli lililoko Wilaya ya Ilemela Jijini Mwanza wamewaomba Wafanyabiashara wenzao walioenda kufanya biashara katika maeneo yasiyo rasmi kurudi kwenye soko hilo kwani kuondoka kwao kumeathiri uchumi wao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti Wafanyabiashara hao wameeleza kwa sasa wanahali ngumu kiuchumi kutokana na idadi kubwa ya Wafanyabiashara kuondoka katika soko hilo hivyo kupelekea vibanda vingi kufungwa na wateja kukosekana.
Aidha wameiomba Serikali kutumia Mamlaka waliyonayo kuwarudisha kweye soko hilo ili mzunguko wa biashara uwe mkubwa.
” Tunaamini Serikali yetu inauwezo wa kuwarudisha wamachinga kwenye maeneo yao rasmi ikiwemo soko letu la Kiloleli na watakaporudi biashara zitachangamka na wateja watakuja kwa wingi”, wamesema
Kwa upande wake Mwenyekiti wa soko hilo Kalala Magafu, ameeleza kuwa awali soko hilo lilikuwa na zaidi ya Wafanyabiashara 1000 lakini walivyoanza kutoka na kwenda kwenye maeneo yasiyo rasmi wamebaki 400.
Amesema licha ya soko hilo kuwa na miundombinu rafiki lakini wafanyabiashara wameondoka na kwenda kwenye maeneo yasiyo rasmi nahivyo kupelekea soko hilo kutochangamka kama ilivyokuwa awali.