Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Mustapher Siyani
Na Tiganya Vincent-Mahakama -Ruvuma
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania , Mhe. Mustapher Mohamed Siyani anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika hafla ya uzinduzi wa majengo ya Mahakama nne za Wilaya tarehe 05 Januari , 2023.
Uzinduzi wa Mahakama hizo utafanyika katika Viwanja vya Mahakama ya Wilaya ya Namtumbo, mkoani Ruvuma.
Uzinduzi huo ni mwendelezo wa ujenzi na uboreshaji wa miradi ya majengo ya mahakama inayoendelea kuzinduziwa nchini.
Majengo hayo ya Mahakama za wilaya yamejengwa kwa fedha za ndani na yatakayozinduliwa kwa pamoja siku hiyo
Miundombinu hiyo imezingatia mahitaji ya kisasa kwa wadau wa mnyororo wa utoaji haki ambapo zipo ofisi za Mawakili, Maafisa Magereza, Ustawi wa Jamii. Watu wenye mahitaji maalum na watoto wamewekewa vyumba vya kutumia wakiwa mahakamani hapo.
Kuzinduliwa kwa majengo hayo kutaongeza ufanisi wa utoaji huduma kwa wananchi kwani yana mazingira rafiki ya utoaji wa huduma kwa wananchi kwa kutumia mfumo ya kitekinolojia.
Huu ni utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama wa Miaka mitano (5) wa 2020/21-2024/25 unahimiza upatikanaji wa haki kwa wakati kupitia uboreshaji wa miundombinu ya majengo na kusogeza huduma za haki karibu na wananchi.
Wananchi wa Mkoa wa Ruvuma wanaombwa kujitokeza katika Viwanja vya Mahakama ya Wilaya ya Namtumbo kushuhudia uzinduzi huo ambao ni ishara ya kuwepo mabadiliko makubwa ya maboresho ya utoaji huduma za Mahakama nchini.