Meneja wa Ruwasa wilaya ya Makete mkoani Mbeya Mhandisi Tanu Deule akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi mpya wa maji wa Ngano unaotarajiwa kunufaisha jumla ya vijiji 25 wilayani humo.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)Mhandisi Clement Kivegalo, akizungumza na wakazi wa kijiji cha Ikolo Halmashauri ya wilaya Kyela mkoani Mbeya baada ya kutambulisha mradi wa maji wa Ngana unaotekelezwa na Ruwasa kwa gharama ya zaidi ya Shilingi bilioni 7.
Mkurugenzi wa Ufundi wa wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)Mhandisi Ndele Mengo na baadhi ya wafanyakazi wa Ruwasa wakimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Ruwasa Mhandisi Clement Kivegalo(hayupo pichani) katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Ikolo wilayani Kyela wakati wa ziara ya Mhandisi Kivegalo kutembelea na kukagua ujenzi wa miradi ya maji mkoani Mbeya.
Mbunge wa Jimbo la Kyela mkoani Mbeya Ali Jumbe,akizungumza na wakazi wa kijiji cha Ikolo wilayani humo.
………………………
Na Muhidin Amri,Kyela
TAKRIBANI vijiji 25 vya wilaya ya Kyela mkoani Mbeya,vinatarajiwa kupata huduma ya maji safi na salama kufuatia wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) kutenga kiasi cha Sh.bilioni 7,999,386,700.00 kwa ajili ya kujenga mradi mkubwa wa maji.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Ruwasa Mhandisi Clement Kivegalo,wakati akitambulisha mradi wa maji Ngana- Group kwa wakazi wa kijiji cha Ikolo wilayani Kyela, akiwa katika ziara ya kukagua na kutembelea utekelezaji wa miradi ya maji mkoani Mbeya.
Alisema katika kumaliza tatizo la maji kwa wananchi hasa wanaoishi maeneo ya vijijini,Ruwasa inaendelea kutekeleza jumla ya miradi 1,029 kwa gharama ya Sh.bilioni 387 kati ya fedha hizo Sh.bilioni 7.9 zitatumika kutekeleza mradi wa maji Ikolo.
Mhandisi Kivegalo,ameishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuendelea kutoa fedha ambazo zinakwenda kumaliza kero ya maji kwa wananchi wa vijiji mbalimbali hapa nchini.
“tunaposema Mama anaupiga mwingi sisi Ruwasa ni mashahidi,katika awamu zilizopita kulikuwa na ujenzi wa miradi ya maji na fedha zilitolewa,lakini sehemu kubwa ya fedha hizo hazikuweza kutekeleza miradi ya maji hata kwa asilimia 50”alisema Kivegalo.
Amewaomba wananchi wa kijiji cha Ikolo na jimbo la Kyela,kuupokea mradi huo na kumtaka mkandarasi kampuni ya M/S Contruction Co. Ltd kufanya kazi usiku na mchana ili mradi ukamilike haraka na wananchi waweze kupata huduma ya maji katika maeneo yao.
Mbunge wa Jimbo la Kyela Ali Jumbe alisema,serikali ya awamu ya sita ndiyo iliyoitendea haki wilaya ya Kyela kutokana na kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwamo fedha za miradi ya maji.
Amewaomba wananchi wa jimbo hilo,kuungana ili kuijenga wilaya yao na kuachana na tabia ya kutengana ambayo inaweza kurudisha nyuma uchumi na maendeleo ya Kyela yenye utajiri mkubwa wa rasilimali.
Amemshukuru Mkurugenzi Mkuu wa Ruwasa Mhandisi Clement Kivegalo, kwa kukubali kutenga fedha kwa ajili ya mradi huo ambao utamaliza kero ya muda mrefu ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa vijiji 25 katika jimbo hilo.
Awali Meneja wa Ruwasa wilaya ya Kyela Tanu Deule alisema,mradi wa maji Ngana ulijengwa kuanzia mwaka 1984-1989 ukihusisha mateki 9 ya kuhifadhi maji,vituo vya kuchotea maji 275 na ujenzi wa banio pamoja na mtandao wa bomba ukilenga khudumia vijiji 25.
Alisema, wakati mradi unajengwa ulipangwa kuhudumia watu 34,740 na ulianza kutoa huduma kwa vijiji 25,lakini huduma ilianza kuzorota kwa baadhi ya vijiji baada ya ongezeko la watu hasa katika mji wa Kasumulu(boda)ambao ina watu ni zaidi ya 10,085.
Deule alitaja baadhi ya vijiji vitakavyonufaika na mradi huo ni Mwalisi,Ushirika,Ikolo,Ngonga,Kasumulu na Lupembe na vitongoji sita vya Njisi,Seko,Kilambo,Mbako,Kilasilo na Ibungu katika kata za Ikimba na Njisi zinazohudumiwa na mamlaka ya maji Kyela-Kasumulu.