Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mh. Anthony Mavunde ameonesha dhamira ya kukuza na kuuendeleza mchezo wa mpira wa wavu katika Jiji la Dodoma kwa kuweka miundombimbu bora ya kuchezea na kuendelea kuandaa mashindano mengi mbalimbali ili kuibua na kuendeleza vipaji vya vijana wa Dodoma Mjini.
Mbunge Mavunde ameyasema hayo jana wakati wa fainali za mashindano ya MAVUNDE VOLLEYBALL CUP 2022/23 zilizofanyika katika uwanja wa Shule Ya Msingi Mlezi Jijini Dodoma.
“Kama ambavyo nimekuwa nikisaidia michezo mingine,hivi sasa pia nitaweka nguvu katika mchezo huu wa mpira wa wavu hasa katika miundombinu ya viwanja na kuandaa mashindano mengi zaidi ili tuuendeleze na kuibua vipaji zaidi.
Kwa hivi sasa mashindano haya ya Mavunde Dodoma yamesajiliwa na Chama cha Mpira wa Wavu Tanzania na yanatambulika nchini kote.
Nimefurahi kuona Timu nyingi zimekuja kutoka nje ya Dodoma kama vile Mkoa Wa Dar es salaam,Kigoma,Iringa na Ruvuma hii ni kuonesha kuwa michezo inaunganisha watu,michezo ni furaha,umoja,mshikamano na ni Ajira pia.
Ahadi yangu kwenu ni kwamba mashindano yanayokuja yatakuwa makubwa zaidi na yenye zawadi nono,hivyo muanze maandalizi mapema”Alisema Mavunde
Katika Mashindano hayo yaliyojumuisha wanawake na wanaume,kwa upande wa Wanawake Timu ya Jeshi Stars kutoka Dar es salaam iliibuka mabingwa kwa mwaka 2022/23 na kwa upande wa wanaume Timu ya NHIF ya Dodoma iliibuka mabingwa.