Kama ilivyo desturi tunapoelekea kufunga mwaka, kunakuwa na shamrashamra za wananchi kufurahia na kuona wanavuka mwaka salama na kuingia mwaka mpya wakiwa salama.
Katika kusherehekea sikukuu hiyo Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama tumejipanga vyema kuhakikisha sikukuu hiyo inasherehekewa kwa amani na utulivu.
Aidha tumejipanga kuhakikisha nyumba za ibada, kumbi za starehe na maeneo mengine yanakuwa na ulinzi wa kutosha ambapo askari Pamoja na vikundi vya ulinzi shirikishi watakuwa katika doria za miguu,na magari kila kona ya jiji na wilaya zote za mkoa huu.
katika kusherehekea sikukuu hizo Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha linatoa angalizo kwa mambo yafuatayo:-
Kwa upande wa upigaji wa fataki, watakaoruhusiwa ni wale tu ambao watakua na vibali na hawataruhusiwawa kufyatua katika makazi ya watu.
Ni marufuku kuwapeleka Watoto kwenye majumba ya starehe yenye vileo.
Ni marufuku waendeshaji wa vyombo vya moto kuendesha wakiwa wamelewa.
Ni marufuku kuchoma matairi, kupanga mawe barabarani wakati wakusherehekea sikukuu hiyo.
Wamiliki wa kumbi za starehe wazingatie masharti ya leseni zao ambazo zinaonyesha muda halisi wa kufunga. Halikadhalika wanapaswa kuzingatia usalama katika maeneo yao na kutojaza watu kupita kiasi.
Pia wananchi wanakumbushwa wasiache nyumba zao bila ya uangalifu pindi wanapokwenda kwenye mikesha.
TUKIO LA WATU WATATU KUFARIKI BAADA YA KUSOMBWA NA MAJI
Pia natoa tahadhari kwa Wananchi katika kipindi hiki ambacho mvua zinaendelea kunyesha kuwa makini ili kuepusha madhara ambayo yanayoweza kutokea.
Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na mvua nyingi zinazoendele kunyesha mkoani hapa kuna matukio ya watu watatu kufariki dunia kwa sababu ya mvua hizo ambao ni Baraka Elias (17) mwanafunzi ambaye alikuwa amechaguliwa kuanza kidato cha kwanza na mkazi wa Losiimingoli Wilaya ya Monduli, Sananda Lekishoni (75) mkazi wa Losimingoli wilaya ya Monduli na Lemali Sayeleki (05) Mwanafunzi wa shule ya Msingi Ranchi, Mkazi wa Olbomba Wilayani Longido.
KUKAMATWA KWA WATUMIWA WANNE WA WIZI GARI.
Katika tukio jingine Jeshi la Polisi mkoani hapa limefanikiwa kukamata watu wanne pamoja na gari moja aina ya Toyota hilux lililoibiwa na madereva ambao walitakiwa kulisafirisha kutoka Mpaka wa Kasumulu kuelekea Nchi Jirani.
Ni kwamba Tarehe 29.12.2022 muda wa saa 04:00 asubuhi katika mtaa wa Shamsi Halmashauri ya jiji la Arusha askari wakiwa doria walifanikiwa kukamata gari hilo ambalo lilikuwa likisafirishwa kwa namba IT 3CD50343065 nakuwekewa namba bandia za usajili wa Nchi Jirani KDA 222H. Aidha uchunguzi wa shauri hili unaendelea ili kubaini mtandao mzima.
Niwaombe wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha katika kuwabaini na kuwafichua wahalifu na uhalifu ili kuendelea kuimarisha amani na utulivu uliopo katika mkoa wetu.Pia niwatakie wananchi wote wa Mkoa wa Arusha heri ya mwaka mpya 2023.
IMETOLEWA NA:
JUSTINE MASEJO-ACP
KAMANDA WA POLISI
MKOA WA ARUSHA