Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akipanda miti katika eneo la chanzo cha maji cha Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) kilichopo Ihumwa ikiwa ni mwanzo wa kampeni aliyoizindua ya upandaji miti kwa lengo la kuikijanisha Dodoma. Jumla ya miti 2000 imepandwa katika eneo hilo leo Desemba 31, 2022.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule akizungumza na wananchi wa Ihumwa (hawapo pichani) wakati wa akiongoza zoezi la upandaji miti katika chanzo cha maji cha eneo la Ihumwa, Mkoa wa Dodoma leo Desemba 31, 2022.
………………………………………..
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ametoa rai kwa wakazi wa Dodoma kuanza kutumia nishati mbadala ili kupunguza ukati wa miti kwa ajili ya matumizi ya kuni na mkaa.
Kauli hiyo imetolewa na Mhe. Rosemary Senyamule alipokua akiongoza zoezi la upandaji miti katika eneo la chanzo cha maji cha Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) kilichopo Ihumwa ikiwa ni mwanzo wa kampeni aliyoizindua ya upandaji miti kwa Mkoa wa Dodoma.
“Leo tupo hapa kutekeleza mpango wa Serikali juu ya utunzaji wa mazingira ikiwa ni mwendelezo wa juhudi zilizoanzishwa na wenzetu. Nitoe rai kwa viongozi wa ngazi zote kuhakikisha tunasimamia maelekezo ya Serikali ya kuzuia ukataji miti bila vibali, tuanze kutumia nishati mbadala kama gesi kwa ajili ya kupikia kama anavyosisitiza rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan” Mhe. Senyamule alisisiza.
Vilevile, Mkuu wa Mkoa ametoa maagizo kwa Wakurugenzi wa Halmashauri zote katika Jiji la Dodoma kuhakikisha kuwa wanasimamia na kuendeleza kampeni ya “Soma na Mti” kwa kuhakikisha kila shule na kila mwanafunzi anakua na Mti wake bila kujali kiwango cha elimu pia amesisitiza kufuatwa kwa Sheria ndogo ndogo zilizowekwa na Jiji kwa kila Kaya kupanda miti mitano kwenye eneo lake na kila anayenunua eneo ahakikishe amepanda idadi hiyo ya miti.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini Mhe. Jabir Shekimweri aambaye ameshiriki kikamilifu kwenye zoezi hilo amesema;
“Dodoma ina maeneo mengi ya wazi yanayohitaji kupandwa miti na sisi kama Jiji tunajitahidi kila kipindi cha msimu wa mvua tunapanda miti na kwa kipindi kilichopita tulifanikiwa kupanda takribani miti 800,000 kwenye maeneo mbalimbali. Upandaji miti kwenye eneo hili utaongeza thamani ya Mji wa Serikali na tuhakikishe madhumuni ya kupanda miti yanaendana na utunzaji wake” Alisisitiza Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe. Shekimweri
Kadhalika, Meneja wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Kati ambao ndio wadau wakubwa kwenye kampeni hii Bw. Mathew Kiondo, amesema mpaka sasa wana miche ya kutosha kwenye vitalu vyao takribani laki 8 hadi 9 inayosubiri kupandwa na mpaka Sasa wameshagawa miche 200,000 kwa wananchi na kuhakikisha kuwa hakutakua na upungufu kwani hata ikiisha hapo kwao, wataagiza kutoka sehemu nyingine.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa DUWASA amesema eneo la chanzo cha Maji cha DUWASA lililopo Ihumwa vijijini, lina ukubwa wa ekari 360 zilizotengwa kwa ajili ya hifadhi na linapatikana visima 15 vya kuzalisha maji ambavyo vinazalisha takribani lita 9,000,000 za maji na katika jitihada za kulihifadhi eneo hili pamoja na chanzo cha maji, Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na ujumbe wake wamepanda miti 2,000 katika eneo hilo.