SERIKALI imetoa shilingi bilioni 3.4 kuendeleza ujenzi wa hospitali tano katika Mkoa wa Ruvuma.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amezitaja hospitali ambazo ujenzi wake unaendelea kuwa ni ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa awamu ya kwanza unaogharimu shilingi bilioni 2.7.
“Ujenzi katika hospitali ya Rufaa unahusisha jengo la wagonjwa wa nje OPD,jengo la mionzi na nyumba ya mtumishi”,alisema.
Amezitaja hospitali nyingine ambazo ujenzi wake unaendelea kuwa ni hospitali za Halmashauri za Nyasa,Mbinga,madaba na Songea.
Hata hivyo amesema hali ya upatikanaji wa dawa,vifaa tiba na vitendanishi kwenye vituo vya kutolea huduma za afya mkoani Ruvuma imefikia asilimia 96.
RC Thomas amesema chini ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita Mkoa umejenga vituo vya afya 12 kupitia fedha za tozo na serikali kuu kwa gharama ya shilingi bilioni 7.8.
Ameongeza kuwa serikali pia imetoa zaidi ya shilingi milioni 856 kujenga nyumba tisa za watumishi wa afya na shilingi milioni 900 zimejenga majengo matatu ya Huduma za dharura (EMD) katika hospitali tatu za Tunduru,Nyasa na Madaba.
Baadhi ya wabunge akiwemo Mbunge wa Jimbo la Nyasa Mhandisi Stella Manyanya ameipongeza serikali kwa kuboresha miundombinu na vifaa katika hospitali ya Nyasa ambazo amesema zimesogeza huduma muhimu kwa wananchi.
Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini.
—