Na. Damian Kunambi, Njombe
Mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe Nathaniel Mgaya amewataka viongozi wote wa jumuiya hiyo kwa ngazi ya matawi na kata kuhakikisha zinaanzisha miradi itakayowasaidia badala ya kuwa ombaomba.
Mwenyekiti huyo ameyasema hayo alipofanya ziara ya siku mbili ya kukutana na viongozi wa kata na matawi yake katika kata sita ambazo ni Ludende, Milo, Mlangali, Lupanga, Lubonde na Madilu huku akiwa ameambatana na kamati ya utekelezaji ya jumuiya hiyo ngazi ya wilaya.
“Mimi ni mwenyekiti mpya ninayeanza majukumu yangu katika jumuiya hii, nimesikitishwa kuona jumuiya hii kutokuwa na vyanzo vya fedha kwa ngazi zote, kitu ambacho kinapelekea tunapokuwa na shughuli mbalimbali za kikazi tuanze kuomba omba hela kwa wadau! Sasa mimi kuomba sijazoea nataka jumuiya yetu ijisimamie yenyewe hivyo nawaagiza kutafuta mashamba yatakayopandwa miti pamoja na vibanda vya kuweka biashara” Amesema Mgaya.
Aidha kwa upande wake Kaimu katibu wa jumuiya hiyo wilaya Salum Mfaume amewaasa viongozi hao kuwa na maadili katika jamii zinazo wazunguka badala ya kufanya vitendo vitakavyowafanya wadharaulike kwani baadhi yao wamekuwa wakishindwa kuelimisha jamii kufanya matendo mema ilhali wao ndo wanaongoza kwa maovu.
“Unakuta kiongozi amelewa na kuanza kufanya vurugu ama kutukana watu hivyo, sasa kwa hali hii unafikili utamuelimisha nini mwananchi wa kawaida na akakuelewa?” Amesema Mfaume.
Naye katibu wa elimu, malezi na mazingira Bazil Makungu akiwataka viongozi wa jumuiya hiyo kwa ngazi zote wanapaswa kuhamasisha wanafunzi kujiunga na shule za sekondari za wazazi ili kuweza kuziendeleza shule hizo na kuwafanya wapate elimu bora.
Amesema shule hizi zilianzishwa na waasisi wetu hivyo wana kila sababu ya kuziendeleza na kuzitunza kwani kwakufanya hivyo kutasaidia watoto kupata elimu na malezi yaliyo bora.