Na Alex Sonna
SIMBA SC imeendelea kupunguza Pointi dhidi ya Vinara Yanga SC baada ya kupata ushindi wa mabao 7-1 dhidi ya Tanzania Prisons mchezo wa Ligi Kuu ya NBC uliopigwa katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Simba SC walianza kupata bao dakika ya 12 likifungwa na John Bocco ,akimalizia pasi ya Kiungo fundi Saidi Ntibazonkiza na katika dakika ya 24 Prisons walipata pigo baada ya Samson Mbangula kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kumchezea rafu mbaya mlinzi wa Simba SC,Henock Inonga.
Licha ya kupata pigo hilo Prisons walisawazisha bao kupitia kwa Mshambuliaji wao Jeremia Juma dakika ya 30 hadi mapumziko timu hizo zilienda zikiwa nguvu sawa.
Kipindi cha pili Simba SC walipata bao la mapema dakika ya 46 likifungwa na yule yule John Bocco kwa kazi nzuri ya Pape Ousmane Sakho na dakika ya 60 Saidi Ntibazonkiza alipigilia msumari wa tatu akimalizia kazi ya Clatous Chama.
Mnamo dakika ya 62 John Bocco akifunga bao la nne kwa Simba huku akipiga Hat-Trick yake ya pili msimu na dakika ya 63 Saidi Ntibazonkiza akafunga bao la tano na bao lake la pili ikiwa mechi yake ya kwanza akiwa na Simba SC.
Simba SC iliendelea kulisakama lango la Prisons katika dakika ya 70 Saidi Ntibazonkiza akapiga Hat-trick yake ya kwanza na ikiwa Hat-Trick ya nne katika Msimu huu wa Ligi Kuu ya NBC dakika ya 88 Shomari kapombe akifunga bao la saba yaani wiki.
Kwa ushindi huo Simba SC wamefikisha Pointi 44 wakizidiwa Pointi 3 dhidi ya vinara wa Ligi hiyo Yanga wenye Pointi 47 huku akiwa na mechi moja Mkononi dhidi ya Mtibwa Sugar.
Mechi nyingine Singida Big Stars imeutumia vyema uwanja wake wa CCM Liti mjini Singida baada ya kuichapa mabao 2-1 Geita Gold FC na kufikisha Pointi 37 nafasi ya nne huku Geita Gold FC wakibaki nafasi ya saba wakiwa na Pointi zao 24.
Ligi hiyo itaendelea kesho kwa Mechi mbili kupigwa katika Viwanja tofauti Vinara Yanga SC watakuwa ugenini kucheza na Mtibwa Sugar uwanja wa Manungu Complex na Azam FC atakuwa katika uwanja wake wa Chamazi Complex kucheza na Mbeya City kutoka jijini Mbeya majira ya saa moja usiku.