*******************
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
SHIRIKA lisilo la kiserikali la AKO Tanzania Community Support limetoa msaada wa kuwalipia bima ya mfuko wa afya ya jamii (iCHF) watoto 326 wa Vijiji vya Kambi ya Chokaa na Losoito, Kata ya Naisinyai, Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.
Mkurugenzi wa AKO Tanzania Hilda Kimath amesema shirika hilo limewalipia watoto hao kiasi cha shilingi milioni moja, laki tisa na elfu hamsini na sita ili wakatiwe bima hiyo.
Kimath amesema kupitia fedha hizo shilingi 1,956,000 zilizotolewa na AKO Tanzania, watoto hao 326 watapatiwa huduma ya afya bila kutozwa fedha pindi wakiugua.
“Baada ya kusikia kuwa kuna changamoto ya watoto hao kupata matibabu pindi wakiugua, AKO Tanzania ilijitolea kuwasaidia na kuwalipia bima hiyo ya iCHF,” amesema Kimath.
Mratibu wa mfuko wa bima ya afya ya jamii iliyoboreshwa (iCHF) Wilaya ya Simanjiro, Ibrahim Yeo amekiri watoto 326 hao wa vijiji hivyo viwili kulipiwa kiwango hicho cha fedha kwa ajili ya bima hiyo.
Yeo amewashukuru viongozi wa shirika la AKO Tanzania kwa kuwalipia kiasi hicho cha fedha watoto hao ambao watapatiwa huduma ya matibabu pindi wakiugua.
Mkazi wa kijiji cha Kambi ya Chokaa, Elias Loshilaa amewashukuru AKO Tanzania kwa kufanikisha jambo hilo kwani watoto hao hivi sasa wana uhakika wa kupata matibabu endapo wataugua.
“Mashirika mengine yasiyo ya kiserikali yaige mfano wa AKO Tanzania kwa namna wanavyohudumia jamii hasa zilizo pembezoni ambazo zina uhitaji mkubwa,” amesema Loshilaa.