Afisa muuguzi ambaye ni Mratibu wa maswala ya ukatili wa kijinsia kutoka hospitali ya Mount Meru ,Lilian Lukumay akizungumza na watoto waishio mazingira hatarishi kuhusu maswala ya ukatili wa kijinsia.
Mwenyekiti wa taasisi ya Vijana kwa pamoja tunaweza(VIPATU) ,Jane Edward akizungumza kuhusiana na semina hiyo ya maswala ya ukatili wa kijinsia
Baadhi ya watoto hao wakipatiwa semina hiyo jijini Arusha
***********************
Julieth Laizer,Arusha.
Arusha .Wazazi pamoja na walezi wametakiwa kuwa karibu na watoto wa kiume pamoja na kuzungumza nao kuhusiana na maswala ya ukatili wa kijinsia kwani wao ndio wanaoongoza kufanyiwa vitendo hivyo.
Aidha wazazi wengi wamekuwa karibu sana na watoto wa kike na kuwasahau watoto wa kiume na hivyo kujikuta wao ndio waathirika zaidi wa vitendo hivyo kutokana na kutokuwa na elimu yoyote.
Hayo yamesemwa jijini Arusha na Afisa muuguzi ambaye pia ni Mratibu wa maswala ya ukatili wa kijinsia kutoka hospitali ya Mount Meru,Lilian Lukumay wakati akizungumza na watoto wanaotoka kwenye mazingira hatarishi wanaolelewa katika vituo mbalimbali ambapo waliweza kupatiwa elimu juu ya maswala ya ukatili wa kijinsia semina iliyoandaliwa na taasisi ya Vijana kwa pamoja tunaweza(VIPATU).
Amesema kuwa, elimu zaidi inatakiwa kutolewa kwa watoto wa kiume kwani ndio waathirika wakubwa wanaofanyiwa vitendo vya ukatili na hii imekuwa ni changamoto kubwa katika maeneo mbalimbali.
“Tunaomba sana wazazi na walezi mkae chini na watoto wenu wa kiume waelezeni swala la ukatili wa kijinsia bila kuwaonea aibu yoyote kwani zamani elimu hiyo ilikuwa ikilenga zaidi kwa watoto wa kike ila kwa sasa hivi hali ni mbaya sana pande zote pindi zimetakiwa kupewa elimu ili wafahamu na kujua madhara take na hatua za kuchukua pindi wanapofanyia vitendo hivyo “amesema .
Aidha ameongeza kuwa,takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 60 ya watoto wanafanyiwa vitendo vya ukatili majumbani huku asilimia 40 wakifanyiwa mashuleni huku ukatili wa kingono ukiongoza zaidi kwa watoto hao.
Mwenyekiti wa Taasisi ya VIPATU ,Jane Edward alisema kuwa, lengo kubwa la kuandaa semina hiyo ni kuwakutanisha watoto hao na kuweza kupata elimu juu ya maswala la ukatili wa kijinsia kwani wengi wao hawana elimu juu ya maswala hayo .
“Tumeamua kuwakutanisha hawa watoto wanaolelewa kwenye vituo mbalimbali pamoja na wale wanaoishi mitaani ili waweze kupata elimu kuhusu maswala hayo kwani wengi wao wamekuwa wakifanyiwa ukatili wa kingono na kukosa sehemu ya kuripoti matukio hayo ,hivyo kupitia elimu hii itawasaidia sana kuchukua tahadhari mapema na kuweza kuwasaidia wenzao kwa ujumla.”amesema Jane.
Jane amesema kuwa, ukatili wa kijinsia unaendelea kushika kasi kwa watoto ambapo wanaofanyiwa zaidi ni wanaume ,hivyo kuyataka mashirika mbalimbali pamoja na wadau kuongeza nguvu katika kusaidia watoto hao ili waweze kuondokana na changamoto mbalimbali ikiwemo za ukatili wanaofanyiwa majumbani na mashuleni.
Baadhi ya walezi wa vituo hivyo,Anna Ismali kutoka kituo cha Grace na Dorcas kutoka kituo cha Moshono wamesema kuwa,wanashukuru sana Taasisi hiyo kwa namna ambavyo imewawezesha kufanyika kwa semina hiyo kwani watoto wengi hawana uelewa wa kutosha juu ya maswala ya ukatili wa kijinsia ,huku wakiomba wadau mbalimbali kufika vituoni na kutoa elimu hiyo ili watoto hao waweze kunufaika na kuokoa kizazi cha kesho.