*****************
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
WALIMU Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wameaswa kujiunga na Chama cha kulinda na kutetea haki za walimu CHAKUHAWATA ili waweze kupata haki zao stahiki.
Kaimu Katibu wa CHAKUHAWATA Mwalimu Costantine Tunch ameyasema hayo wakati akielezea mikakati mbalimbali ya kuimarisha chama hicho cha kuwatetea walimu kwenye eneo hilo.
Mwalimu Tunch amesema hadi hivi sasa chama hicho Wilayani Simanjiro kina wanachama 62 wa shule mbalimbali waliojiunga kupitia matawi yao.
“CHAKUHAWATA kuna maslahi makubwa kwani mwanachama anakatwa shilingi 5,000 pekee kwa mwezi tofauti na vyama vingine vinavyokata asilimia mbili ya mshahara kwa kila mwezi,” amesema Mwalimu Tunch.
Amesema wanachama wao ni walimu hivyo hawachagui mwalimu wa shule ya sekondari au ya msingi na wanamshukuru mwajiri wao kwa kuwapa nafasi walimu ya kujiunga na chama wanachokipenda.
“Katibu mkuu wa CHAKUHAWATA T.K. Nyamkunga aliandika barua ya kutambulisha chama chetu mkoani April mosi mwaka 2022 hivyo walimu wasiwe na hofu ya kujiunga nasi,” amesema Mwalimu Tunch.
Amesema chama hicho kinatambuliwa kwani kimesajiliwa kwa mujibu wa sheria ya ajira na mahusiano kazini ya mwaka 2004 kifungu cha 48 na kifungu kidogo cha (5).
“Chama chetu kina kanuni, katiba na hati ya kusajiliwa hivyo walimu wajiunge kwani tunamuheshimisha mwalimu akijiunga na chama anachokitaka kwani CHAKUHAWATA kina uwezo wa kusimamia na kutetea maslahi ya walimu,” amesema.
Hata hivyo, mwalimu Tunch amesema CHAKUHAWATA Simanjiro inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo baadhi ya walimu kukosa ufahamu juu ya sheria ya ajir ana mahusiano makazini.
“Kutofahamu hilo kumesababisha baadhi ya walimu kuwa na hofu na uoga hivyo kudhani kuwa wakijiunga na CHAKUHAWATA watakuwa wamemkosea mwajiri wao kumbe sivyo,” amesema Tunch.
Amesema walimu hao hawafahamu mipaka au tofauti ya mwajiri na chama cha wafanyakazi, kwani mwajiri wao hawezi kuwachagulia kuwa wanachama wa chama cha kuwatetea zaidi ya wao wenyewe kuamua.
“Pia chama hakijaimarika kiuchumi kwani bado hatujatoa ajira kwa nafasi zinazotakiwa na hatujafika maeneo mengi ya Wilaya ya Simanjiro katika kuwafikia wanachama,” amesema Tunch.
Amewapongeza viongozi wakuu wa kitaifa wa CHAKUHAWATA Mwenyekiti na Katibu kwa kuimarisha chama chao kwani pamoja na ugumu wa kiuchumi uliopo wamefanikiwa kufika kwenye mikoa na wilaya mbalimbali nchini.