************
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza limethibitisha kutokea kwa tukio la Mtoto Emmanuel Michael kushambuliwa na kuliwa na fisi wakati alipokwenda kuogeshwa mtotoni na dada yake.
Akizungumza leo Alhamisi Disemba 28, 2022 na waandishi wa habari ofisini kwake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbroad Mutafungwa amesema tukio hilo lilitokea Disemba 27, 2022 majira ya saa kumi na mbili jioni katika Kijiji cha Mwangika,tarafa ya Ngula,Kata ya Mwabemba,Wilaya ya Kwimba Mkoani hapa.
Amesema dada wa Emmanuel Michael aitwaye Marry Michael (14) ambae ni mwanafunzi wa darasa la Saba shule ya msingi Mwangika alikwenda mtoni kuwaogesha wadogo zake watano ndipo ghafla alitokea fisi mkubwa na kuanza kuwashambulia.
“Jitihada za binti huyo kutaka kuwaokoa wadogo zake zilishindikana kwani fisi alimzidi nguvu na baadae alimng’ata mtoto huyo mkono wake wa kulia na kukimbia nae porini”, amesema Mutafungwa.
Aidha, amesema kuwa Jeshi hilo kwakushirikiana na idara ya wanyamapori pamoja na wananchi limefanya msako mkali na kufanikiwa kupata baadhi ya mabaki ya viungo vya mtoto huyo na nguo alizokuwa amevaa huku jitihada za kumsaka fisi huyo zikiendelea ili kuhakikisha anadhibitiwa asiendelee kuleta madhara kwa wananchi.
Mwisho Jeshi hilo limewataka wananchi kuchukua tahadhari na uangalizi wa karibu kwa watoto wao katika maeneo hatarishi ili kuwaepusha na vifo,majanga yanayoweza kuepukika.