Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kuanzia Disemba mosi, 2022 hadi Disemba 23, 2022 lilifanya misako ya nguvu na yenye tija katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya na kupata mafanikio yakiwemo kukamata watuhumiwa 45 wa makosa ya kupatikana na Meno ya Tembo, kupatikana na silaha bila kibali, kupatikana na bhangi, kupatikana na bidhaa mbalimbali zilizopigwa marufuku nchini na watuhumiwa wa matukio ya mauaji na kuvunja nyumba na kuiba wamekamatwa:-
KUPATIKANA NA NYARA ZA SERIKALI [MENO YA TEMBO].
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia ELIAS RAULENT @ KAYUTI [50] Mkazi wa Makongolosi akiwa na vipande vitano vya meno ya Tembo vyenye uzito wa Kilogram 18.5 na thamani ya Tshs. 34,950,000/= akiwa ameficha kwenye Begi jeusi. Mtuhumiwa ni muwindaji haramu, atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi wa shauri hili kukamilika. Mtuhumiwa amefikishwa mahakamani na kufunguliwa kesi ya uhujumu uchumi namba 18/2022 [ECO NO.18/2022].
KUPATIKANA NA BIDHAA ZILIZOPIGWA MARUFUKU NCHINI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia 1. LUSEKELO MBEMBELA [45] Mkazi wa Kiwanja Chunya na 2. CHARLES DAUD [34] Dereva Bodaboda, Mkazi wa Tembela Mbeya kwa tuhuma za kupatikana na bidhaa (vipodozi) za aina mbalimbali zenye viambata sumu vilivyopigwa marufuku nchini.
Watuhumiwa walikamatwa Disemba 22, 2022 majira ya saa 05:00 usiku huko Kitongoji cha Chalangwa, Tarafa ya Kiwanja, Wilaya ya Chunya na kukutwa na bidhaa hizo ambazo ni:-
- Beoution Dazan 01 na nusu
- Betasol 120
- Diana 120
- Miki Clair Dazan 02 na nusu
- Whitemax Dazan 04
- Pricence Clear Dazan 10
- Cocopulp ndogo dazan 40
- Cocopulp kubwa dazan 02 @ 24
- Decret write lotion dazan 03 @ 36
- Extra Clair 24
- Citroright 26
- Elegance Clair 03
- BB Ckair 01
- Cocopulp Gricerin 79
- Pawpaw Gricerin 06
- Miki kubwa 06
- Pawpaw 02
- Glu white 02
- Derma Clair 20
- Betasol 30
- Beution Griceli 12.
KUPATIKANA NA MALI ZA WIZI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa wawili 1. HAJI SAID [41] Mkazi wa Ihanga na 2. FIKIRI BARTON [19] Mkazi wa Igawa wilaya ya Mbarali kwa tuhuma za kupatikana na mali za wizi ambazo ni Pikipiki nne [04].
Watuhumiwa walikamatwa Disemba 20, 2022 majira ya saa 08:00 usiku huko maeneo ya mji mdogo wa Rujewa na Igawa, Wilaya ya Mbarali na kukutwa na Pikipiki nne, mbili aina ya Kinglion, moja aina ya TVS na moja aina ya Honlong zote zikiwa hazina Plate namba.
KUPATIKANA NA POMBE HARAMU YA MOSHI [GONGO].
Katika muendelezo wa misako na doria zenye tija, pia Jeshi la Polisi lilifanikiwa kumkamata TUNSUME MBASI MWAIJUMBA [49] Mkazi wa London “B” Wilaya ya Rungwe akiwa na Pombe Haramu ya Moshi @ Gongo lita 20 pamoja na pombe kali zilizopigwa marufuku kuingizwa nchini kutoka nchini Malawi aina ya Ridder boksi 01, Win boksi 01, Ice Dry London Gin boksi 01.
KUPATIKANA NA DAWA ZA KULEVYA.
Katika misako hiyo iliyofanyika katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Mbeya, jumla ya watuhumiwa 06 wa kupatikana na dawa za kulevya aina ya Bhangi walikamatwa wakiwa na bhangi kilogramu 10 na gramu 174.
Watuhumiwa waliokamatwa ni:-
- JONS EDGER [18] Mkazi wa Maanga
- JAMES MWALUPINDI [21] Mkazi wa Ilemi
- ERASTO UKALI [23] Mkazi wa Ubaruku
- AMBAKISYE MWALIYAE KALINGA [63] Mkazi wa Izumbwe
- EMMANUEL GODWIN MWAMBEGELE [32] Mkazi wa Kasanga
- MASKODA JOEL @ MWAIPUNDU [20] Mkazi wa Kasakalawe
KUKAMATWA KWA WATUHUMIWA WANAOJIHUSISHA NA MATUKIO YA WIZI WA SIMU.
Katika misako iliyofanyika Disemba 20, 2022 huko maeneo ya Mapelele, Jijini Mbeya, tulifanikiwa kuwakamata watuhumiwa 04 kwa tuhuma za kujihusisha na matukio ya wizi wa simu za mkononi katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Mbeya.
Watuhumiwa waliokamatwa ni:-
- NICHOLAUS JOHN [26] Fundi Ujenzi, Mkazi wa Nzovwe
- HUMPHREY JOHN [30] Fundi Umeme, Mkazi wa Mbalizi
- NICHOLAUS MASHAKA [24] Kinyozi, Mkazi wa Mapelele
- GREYSON MWINUKA [27] Kinyozi, Mkazi wa Nsalaga
Watuhumiwa walipekuliwa na kukutwa na mali za wizi simu 03 aina ya Infinix Hot 10 mbili na Tecno 01 zote Smartphone.
KUPATIKANA NA SILAHA BILA KIBALI.
Katika misako iliyofanyika huko Wilaya ya Chunya, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanikiwa kuwakamata watuhumiwa 1. DAMIAN THOMAS @ KISANGA [40] Mkazi wa Mwaoga na 2. TIZO NELSON [34] Bodaboda, Mkazi wa Makongolosi wakiwa na silaha aina ya Gobole lililotengenezwa kienyeji na silaha nyingine tatu aina ya Gobole zilizotengenezwa kienyeji, risasi 50 pamoja na fataki 32.
Aidha katika kipindi cha kuanzia Disemba 01, 2022 hadi Disemba 23, 2022 jumla ya watuhumiwa wa matukio ya mauaji 12 walikamatwa ambapo kati yao 05 walifikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.
Mafanikio ya Kesi Mahakamani.
Kwa kipindi cha kuanzia tarehe 01/12/2022 hadi tarehe 23.12.2022 jumla ya kesi 219 zilifunguliwa mahakamani huku kesi 56 zikipata mafanikio ikiwemo washitakiwa kufungwa jela miaka 30 zikiwemo za mauaji na kupatikana na nyara za serikali.
Kosa: Kupatikana na nyara za serikali (Nyama ya Tandara, nyama ya Swala na mifupa ya Mbuni) Watuhumiwa katika mashauri haya walikuwa 1. FIKIRI SHEGA ECO 05/2021 alikutwa na hatia na kuhukumiwa kifungo miaka 20 gerezani, 2. LUCAS BALTON alikutwa na hatia na kuhukumiwa kifungo miaka 20 gerezani, 3. CHRISTOPHER MWANKINA alikutwa na hatia na kuhukumiwa kifungo miaka 20 gerezani na 4. GERVAS KINYAGA alikutwa na hatia na kuhukumiwa kifungo miaka 20 gerezani.
WITO:
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi wa Polisi Benjamin Kuzaga anatoa wito kwa wananchi/wafanyabiashara kuacha kujihusisha na biashara haramu, biashara za magendo na uingizaji wa vipodozi vilivyopigwa marufuku nchini kwani ni kinyume cha sheria na badala yake watafute biashara halali ili wajipatie kipato halali na kufanya biashara zao kwa uhuru.
Aidha anatoa wito kwa jamii kuacha kujihusisha na uhalifu vinginevyo Jeshi la Polisi halina huruma na yeyote atakayebainika kujihusisha na uhalifu kwani atakamatwa na kufikishwa mahakamani na kutumikia vifungo mbalimbali.
Pia anatoa wito kwa wananchi walioibiwa Pikipiki kufika kituo cha Polisi Rujewa Mbarali na wale walioibiwa simu za mkononi kufika kituo cha Polisi Central Mbeya wakiwa na nyaraka zinazoonyesha uhalali wa kumiliki mali hizo kwa ajili ya utambuzi na taratibu za kurejeshewa mali zao.
Imetolewa na,
ACP Benjamin E. Kuzaga
Kamanda wa Polisi,
Mkoa wa Mbeya.