Na Hellen Mtereko, Mwanza
Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza limeitaka jamii kuachana na dhana potofu iliyojengeka kuwa mwisho wa mwaka huwa na matukio mabaya yanayohusisha vifo,uhalifu na ajali za barabarani badala yake waishi kwa kufuata sheria,mila,desturi na tamaduni za nchi.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumamosi Disemba 24, 2022 na Kamanda wa Polisi Mkoani Mwanza Wilbroad Mutafungwa, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.
Kamanda Mutafungwa amesema kuwa inapofika wakati wa sikukuu mambo mengi hujitokeza yakiwemo ya kihalifu lakini kutokana na Jeshi hilo kujipanga ki sawa sawa hategemei kuona matendo maovu yakijitokeza huku akiwaonya watu wenye nia ya kuhatarisha usalama kuwa wataishia kukamatwa na Jeshi hilo.
” Katika kuelekea sikukuu za Krismas na mwaka mpya, nitoe onyo kwa wote watakaojihusisha na uchomaji wa matairi Barabarani wakati wa sherehe hizo, tabia ya kuendesha magari huku wamelewa pombe pamoja na upigaji wa baruti ambazo zinaweza kuleta taharuki kwa jamii na kupelekea kuhatarisha maisha ya watu”, amesema
Aidha, Kamanda Mutafungwa amepiga marufuku suala la disco toto huku akiwasihi wazazi kuwa karibu na watoto wao sanjari na kutowaruhusu kwenda kwenye mikusanyiko ya watu ili kuepukana na changamoto ya kupotea kwa watoto.
Ameongeza kuwa Jeshi hilo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama watahakikisha waumini na wananchi wote wa Mkoa wa Mwanza wanasherekea sikukuu hizo kwa amani na utulivu.
Kamanda Mutafungwa amewaomba Wananchi kuchukua tahadhari kwenye miji yao wanapokuwa wanaenda kweye mkesha wa sikukuu hizo ikiwa ni pamoja na kuacha mtu nyumbani kwaajili ya ulinzi na usalama wa mali zao.