Mchungaji wa Kanisa la EAGT Kiloleli Jacob Mutashi akizungumzia namna ya kusherekea sikukuu za Krismas na mwaka
Mchungaji Jacob Mutashi akisoma maandiko
*******************
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Jamii imetakiwa kusherekea sikukuu za Krismas na mwaka mpya kwa amani na utulivu hatua itakayosaidia kuepukana na changamoto mbalimbali ikiwemo ya kukamatwa na Jeshi la polisi.
Rai hiyo imetolewa leo Disemba 24 na Mchungaji wa Kanisa la E.A.G.T Kiloleli lililoko Jijini Mwanza Dkt Jacob Mutashi, wakati akizungumza na waandishi wa habari
Amesema jamii isitumie sikuku kufanya mambo ambayo hayampendezi mwenyezi Mungu badala yake wajikite kwenye maombi sanjari na kukaa na familia zao kwaajili ya kusherekea sikukuu kwa amani na utulivu.
Mutashi amesema Krismas ni kumbukizi ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo hivyo inapaswa kusherekea kwa utulivu na unyenyekevu mkubwa kutokana na sikukuu hiyo kuwa maalumu na takatifu.
” Ibada zimekuwa zikifanyika katika nyumba mbalimbali za kuabudia ila baada ya hapo watu wakitoka wanaenda kujichanganya kwenye nyumba za starehe kwaajili ya kusherekea jambo ambalo halitakiwi katika Imani za kikiristo”, amesema
Aidha, amewaomba wazazi kukaa karibu na watoto wao kipindi hiki cha sikukuu ikiwa ni pamoja na kutowaruhusu kwenda kwenye disko toto kwani ndio njia moja wapo ya watoto kujifunza na kuiga tabia mbaya ambazo zinaweza kupelekea kukatisha ndoto zao.
” Disko toto zimekuwa zikiwakutanisha watoto kutoka familia tofauti tofauti na kila mtoto anatabia yake kulingana na malezi aliyolelewa na wazazi wake hivyo wanapokutana pamoja wanafundishana tabia ambazo siyo nzuri na wengine hata kulawitiana hivyo wazazi epukeni sana kuruhusu watoto kweda kwenye disko toto”, amesema Mchungaji Mutashi
Mchungaji Mutashi amemuomba Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani hapa kufuta disko toto kwani ndio chanzo cha mmomonyoko wa maadili na zinachochea kuharibu malezi ya watoto.