Wizara ya Afya imewataka watumiaji wote wa vyombo vya moto barabarani katika kipindi hiki cha kuelekea sikukuu ya krismasi, mwisho wa mwaka na mwaka mpya kuchukua tahadhari ili kuepuka ajali zinazosababisha vifo, ulemavu wa kudumu na kuipa Serikali mzigo mkubwa wa kuhudumia wahanga.
Hayo yamesemwa leo na Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Prof. Abel Makubi alipofanya ziara katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na kutembelea wodi za wagonjwa wa upasuaji ambapo zaidi ya asilimia 70 ni wagonjwa wa ajali.
Amewaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa nchini kushirikiana na Jeshi la Polisi, Kitengo cha Usalama Barabarani kuwapima madereva afya ya mwili na akili ili wanaogundulika kuwa na tatizo waende hospitali kupata tiba stahiki na kuendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa vyombo vya moto ili vile vitakavyobainika kuwa na hitilafu vizuiwe kutoa huduma kwani ajali zinapotokea kazi kubwa inahamia hospitalini.
Takwimu kutoka Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) zinaonesha kuwa katika kipindi cha Aprili hadi Juni, 2022 wagonjwa wa ajali walikua 1,917 na kipindi cha Julai hadi Septemba, 2022 wagonjwa wa ajali walikua 2,410, hivyo katika vipindi viwili hivyo asilimia 70 zilikua ajali za barabarani. Takwimu hizo kutoka hospitali moja tu zinaonesha ongezeko la ajali 493.
Gharama za kutibu wagonjwa wa ajali MOI waliopata mivunjiko ya mifupa mirefu (fracture) na kulazimika kufanyiwa upasuaji na kuwekewa vyuma (implants) hugharimu takribani shilingi milioni mbili ambapo wagonjwa waliopata ajali na kuumia kichwani hasa ubongo (Traumatic Brain Injury) na kulazimika kufanyiwa upasuaji, hugharimu kiasi cha shilingi milioni 6 hadi 20 kutokana na kuhitaji huduma ya ICU baada ya upasuaji na kukaa hospitali wastani wa siku 20. Asilimila 60 ya wagonjwa hawa, hawana bima ya afya, hushindwa kulipia huduma waliyopata hivyo Serikali hubeba mzigo huu wa matibabu ambao ni mkubwa na haiwezi kuendelea kuubeba.
Katika hatua nyingine, Prof. Makubi ameleeza kuwa Wizara imejipanga kuwa na magari ya kutosha ya dharura kwa wagonjwa ili ajali zinapotokea yaweze kutumika na tayari Serikali imenunua magari zaidi 660 yatakayosambazwa nchi nzima na yanatarajiwa kufika nchini mwezi Juni 2023.
Kutokana na hatua hiyo, Prof. Makubi amesema Wizara itakua na mfumo wa kuweza kufahamu gari la wagonjwa liko wapi ili ajali inapotokea gari hilo liweze kufika mapema eneo la tukio kuchukua majeruhi kwa ajili ya matibabu zaidi.